Michezo

Lampard alia Chelsea walinyimwa penalti katika sare tasa waliyosajili dhidi ya Manchester United ligini

October 25th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Frank Lampard ameshikilia kwamba kikosi chake cha Chelsea kilistahili kupokezwa penalti baada ya beki Cesar Azpilicueta kuchezewa visivyo na Harry Maguire katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowakutanisha na Manchester United mnamo Oktoba 24, 2020, ugani Old Trafford.

Azpilicueta ambaye ni nahodha wa Chelsea alikabiliwa kivoloya na Maguire aliyemkwida shingoni wakati wakiwania mpira ndani ya kijisanduku.

Licha ya tukio hilo kurejelewa na teknolojia ya VAR, hakuna penalti ambayo Chelsea walipokezwa na Maguire hakuadhibiwa.

“Nilidhani ingekuwa penalti ya moja kwa moja ikizingatiwa jinsi ambavyo Azpilicueta alikabiliwa,” akatanguliza Lampard.

Matokeo hayo yalisaidia Man-United kuepuka kichapo cha tatu mfululizo katika uwanja wao wa nyumbani kwa mara ya kwanza tangu 1930.

Mchuano huo ulimpa kipa mpya wa Chelsea, Edouard Mendy, jukwaa zuri la kudhihirisha umahiri wake katikati ya michuma baada ya kuwanyima Marcus Rashford na Bruno Fernandes nafasi nyingi za wazi.

Hata hivyo, nusura ajichongee mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya pasi fupi aliyolenga imfikie beki Thiago Silva kufikiwa kirahisi na Rashford.

Edinson Cavani, aliwajibishwa kwa mara ya kwanza na Man-United na akashirikiana vilivyo na Paul Pogba na Mason Greenwood.

Mbali na Mendy, sajili wapya wengine walioridhisha zaidi kambini mwa Chelsea ni Silva na Timo Werner ambaye kwa pamoja na Christian Pulisic, walitatiza sana safu ya nyuma ya Man-United.

Ni mara ya kwanza tangu 1972-73 kwa Man-United kukosa kusajili ushindi katika mechi tatu za EPL uwanjani Old Trafford.

Man-United kwa sasa wanajiandaa kuvaana na RB Leipzig ya Ujerumani kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Oktoba 28 kabla ya kuwaalika Arsenal kwa gozi kali la EPL ugani Old Trafford mnamo Novemba 1, 2020.

Kwa upande wao, Chelsea watasafiri Urusi kuchuana na FK Krasnodar katika mechi ya pili ya UEFA mnamo Oktoba 28 kabla ya kushuka dimbani kupepetana na Burnley ugani Turf Moor mnamo Oktoba 31, 2020.