Michezo

Lampard aridhika na sare dhidi ya Ajax katika Uefa

November 7th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA Frank Lampard amewapongeza vijana wake kwa juhudi zao zilizowafanya waagane kwa 4-4 na Ajax Amsterdam baada ya kuwa chini kwa 4-1 katika pambano lao la Ligi ya Klabu Bingwa, matokeo ambayo yamewaongezea matumaini ya kutinga hatua ya 16 Bora.

Chelsea walicheza vibaya kwenye mechi hiyo mbele ya mashabiki wao ugani Stamford Bridge, Jumanne usiku.

Ajax waliongoza kwa mabao hayo kutokana na mabao ya Hamim Ziyech, Donny van de Beek pamoja na mengine ya kujifunga kupitia kwa kipa Arrizabalaga na mshambuliaji Tammy Abraham.

Nahodha Cesar Azpilicueta aliifungia Chelsea bao la kwanza katika mechi hiyo ambayo mashabiki walishuhudia mabeki wa Ajax, Daley Blind na Joel Veltman wakilishwa kadi nyekundi. Kiungo mahiri aliongeza mabao mengine mawili ya mikwaju ya penalti kupitia kwa Jorginho.

Kinda Reece James mwenye umri wa miaka 19 aliifungia Chelsea bao la kusawazisha baada ya kuilemea ngome ya Ajax ambayo ilikuwa imefifia kufuatia kuondolewa kwa Blind na Veltman.

Azpilicueta alifungia Chelsea bao la tano lakini likakataliwa na mtambo wa kiteknolojia wa VAR uliobuniwa kumsaidia mwamuzi kutoa uamuzi kunapotokea ubishi uwanjani.

“Nawapa heko vijana wangu kwa kucheza kwa bidii hata walipokuwa chini kwa 3-1 kufikia wakati wa mapumziko; na hata 4-1.”

Matokeo hayo yameiweka Chelsea sawa na Ajax, kila moja ikiwa na pointi saba, kila moja ikiwa imebakisha mechi mbili kukamilisha mechi za kundini.

Valencia ambao waliibuka na ushindi wa 4-1 dhidi ya Lille, watakutana na Chelsea baadaye mwezi huu wa Novemba.

“Daima nilisema tutapata upinzani mkali katika kundi hili. Tuna nafasi kubwa ya kufuzu, lakini lazima tuzidi kujitahidi zaidi. Tungali na mechi mbili, ugenini dhidi ya Valencia na hapa nyumbani dhidi ya Lille. Zote ni mechi ngumu. Nilitarajia ushindi leo, lakini wapinzani wetu pia walikuwa wamejiandaa vyema kuzua upinzani mkali,” alisema kiungo huyo mstaafu.

“Kumbukeni, Valencia wamepata ushindi mkubwa leo usiku na kujiongezea matumaini ya kufuzu kwa 16 Bora,” aliongeza ambaye timu yake ilipata pigo baada ya kinda Mason Mount kuumia.

Nafasi ya chipukizi huyo ilichukuliwa na Reece ambaye alicheza vizuri na kufunga bao la kusawazisha.

Matokeo ya mechi za Jumanne kwa ufupi yalikuwa:

Liverpool 2 Genk 1

Napoli 1 Red Bull 1

Valencia 4 Lille 1

Chelsea 4 Ajax 4

Lyon 3 Benfica 1

Borussia Dortmund 3 Inter Milan 2.