Michezo

Lampard arukia vijana kupepetwa na Bayern

February 27th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Frank Lampard wa Chelsea amewalaumu wachezaji wake kwa uzembe walioufanya dhidi ya Bayern Munich katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kucharazwa 3-0, Jumanne usiku.

Kiungo huyo mstaafu alisema wachezaji wake walifanya uzembe uliowapa Bayern nafasi ya kupata mabao hayo kirahisi katika kipindi cha pili.

Kauli kama hiyo vilevile imetolewa na wanasoka wastaafu waliokuwa wachambuzi wa mechi hiyo iliyochezewa Stamford Bridge, mbele ya mashabiki wao wengi waliomiminika uwanjani humo kushuhudia pambano hilo la mkondo wa kwanza.

Baada ya kucheza vizuri, mabeki wa Chelsea walifanya makosa kadhaa katika kipindi cha pili ambayo yalimwezesha Serge Gnabry kufunga mabao mawili, kabla ya Robert Lowendowski kufunga la tatu.

“Usiku umekuwa mgumu kwa baadhi ya wachezaji wangu ambao nilishuhudia wakifanya makosa,” alisema Lmapard ambaye alikuwa kiungo mahiri ya Chelsea na pia timu ya taifa ya Uingereza.

“Ni kawaida mchezaji mzuri anaweza kufanya makosa uwanjani, lakini pia kuna vile anaweza kuzuia kuyafanya,” alisema.

Hata hivyo, kocha huyo alimsifu kiungo Mateo Kovacic kutokana na kiwango chake cha juu kwenye mechi hiyo.

“Kuna wale waliojitahidi, hasa Kovacic, aliyecheza kwa staha na kiwango cha juu. Lakini shida yetu kuu ilikuwa kutojiamini kwa baadhi ya wachezaji ambao walipata nafasi kikosini.”

Lampard ambaye alikisifu kikosi cha Bayern kutokana na kiwango chao bora, alisema vijana wake wana kibarua kigumu katika juhudi za kubadilisha matokeo hayo ya 3-0, timu hizo zitakaporudiana katika uwanja maarufu wa Allianz Arena hapo Machi 18.

Safu ya Bayern chini ya Thiago Alcantara ilicheza kwa ushirikiano mkubwa huku akiitekeleza kazi yake ya kusambaza mipira vyema, ingawa alitatizwa na Kovacic mara kwa mara.

Kiungo mshambuliaji Thoma Muller mwenye umri wa miaka 29.