Michezo

Lampard kukosa vifaa akikabili Newcastle

October 17th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA Frank Lampard huenda akaunda kikosi chake bila nyota kadhaa walioumia katika mechi za kimataifa.

Chelsea wamepangiwa kukutana na Newcastle United Jumamosi, lakini huenda wakacheza bila Andreas Christensen na Mateo Kovacic.

Lakini klabu hiyo imethibitisha kwamba kiungo mzuiaji N’Golo Kante atakuwa kikosini, hata baada ya kuondolewa kikosini Ufaransa kabla ya Ufaransa kucheza na Iceland.

Lampard ana imani kiungo huyo wa zamani wa Leicester City atakuwa fiti kucheza dhidi ya Newcastle United mnamo Oktoba 19.

Kante aliumia muda mfupi kabla ya mechi hiyo, lakini kocha Didier Deschamps alisema alifanya hivyo kama tahadhari.

Nafasi ya kiungo huyo ilichukuliwa na Moussa Sissoko wa Tottenham ambapo Ufaransa iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

“Alikuwa anasikia maumivu kidogo ya msuli. Alisema Deschamps baada ya mechi hiyo.

“Alikuwa anasikia maumivu ambayo yalimfanya asijisikie kucheza. Nilifanya uamuzi wa kumuondoa kikosini kwa sababu angeumia zaidi na nikampa nafasi hiyo Moussa ambaye nilijua alikuwa tayari kucheza,” kocha aliongeza.

“Sikudhani kama hali yake ingekuwa mbaya zaidi kwake, lakini sina uhakika kama ataweza kurejea mapema,” aliongeza.

Kante ameanza kwenye mechi nane za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kusumbuliwa na jeraha la kifundo cha mguu hapo awali.

Jeraha hilo lilimkosesha mechi kadhaa, ikiwemo ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Valencia.

Chelsea ambayo inashikilia nafasi ya tano kwa sasa iko nyuma ya vinara Liverpool kwa tofauti ya pointi 10 baada ya kucheza mechi nane, ikiwa na tofauti ya pointi mbili tu nyuma ya Manchester City wanaoshika nafasi ya pili jedwalini.

Wakatiu huo huo, kipa Alisson Becker wa Livepool aliyeumia wakicheza na Norwich amepata nafuu na sasa yuko tayari kuendelea kulinda lango mabingwa hao wa Klabu Bingwa barani Ulaya.

Klabu yake ilithibitisha jana kwamba mlinda lango huyo matata atakuwa langoni Jumapili Liverpool itakapokabiliana na Manchester United, ugani Old Trafford.

Liverpool ambao wamo kileleni mwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wamekuwa bila kipa huyo chaguo la kwanza mwenye umri wa miaka 27 tangu aumie katika mechi hiyo ya kufungua msimu.

Alisson amekuwa akifanya mazoezi makali bila kusimamiwa kwa wiki moja na madaktari wamethibitisha kwamba yuko katika hali nzuri ya kuchukua nafasi yake ambayo ilikuwa ikijazwa na Arian, ambaye pia amethibitisha uwezo wake.

Tangu akabidhiwe usukani, Levrpool imehifadhi rekodi yake ya asilimia 100 tangu msimu huu uanze, matokeo ambayo yamempa kocha Jurgen Klopp matumaini makubwa ya kushinda taji telezi kwake la EPL.

Mshambuliaji Mohamed Salah ambaye pia aliumia kisigino wakicheza na Leicester City, pia anatarajiwa kurejea Jumapili kuvuruga Manchester United.