Raila aahidi kuigeuza Lamu iwe ‘Dubai ya Afrika’

Raila aahidi kuigeuza Lamu iwe ‘Dubai ya Afrika’

Na KALUME KAZUNGU

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga, ameahidi kusukuma kuanzishwa kwa viwanda vikubwa vikubwa Lamu na kulibadilisha eneo hilo kuwa ‘Dubai’ ya Kenya na Afrika kwa ujumla.

Akihutubia umma kwenye maeneo ya Mpeketoni, Witu na Mkunguni wakati wa ziara yake katika Kaunti ya Lamu, Bw Odinga alisema atatumia cheo chake cha afisa wa Miundomsingi na Maendeleo katika Muungano wa Afrika (AU) kusukuma ujenzi wa njia ya reli itakayounganisha bahari ya Atlantic na Bahari Hindi eneo la Lamu ili kuwezesha bidhaa kutoka Dubai, Japan na sehemu nyingine za ulimwengu kuingizwa au kutoka Lamu.

Alitaja Bandari ya Lamu (Lapsset) kuwa kitovu cha biashara kwa Lamu, Kenya na ulimwengu kwa ujumla na akaahidi kuhakikisha ujenzi wa viegesho vilivyobakia vya Lapsset unakamilika ili kutoa ajira kwa vijana wengi wa Lamu na Kenya.

Alisema azma yake pia ni kuona kwamba uchumi wa baharini, hasa uvuvi unaimarishwa zaidi kupitia ujenzi wa viwanda vya samaki kuwezesha samaki hao kuvuliwa baharini na kupitia uboreshaji Lamu kabla ya kuuzwamataifa ya ng’ambo.

“Hapa tuko na Lapsset ambayo ujenzi wa viegesho vitatu vya kwanza unaendelea. Cha kwanza tayari kimekamilika na shughuli za kibiashara zinaendelea. Msimamo wangu ni kuona kwamba viegesho vyote 32 vinakuwa tayari ili ajira kwa vijana iwepo,” akasema Bw Odinga.

Akaongeza, “Badala ya kuacha mataifa kama vile China kuvamia bahari yet una kuvua samaki na kwendanao ng’ambo, azma yangu ni kuanzisha kiwanda kikubwa hapa Lamu.Tunataka kuona kuwa samaki wanavuliwa baharini na kupitia uboreshaji ili watu kutoka Afrika Kusini,Dubai na sehemu zingine wananunua samaki hao hapa kwetu Lamu,” akasema Bw Odinga.

Akigusia kuhusu Azimio La Umoja, Bw Odinga aliwasihi wakazi wa Lamu na Wakenya kwa ujumla kudumisha amani, usawa, upendo, ushirikiano na utangamano wakati huu ambapo taifa linajiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Aliwaonya wananchi dhidi ya kupotoshwa na wanasiasa wabinafsi.

Naye Gavana wa Lamu, Fahim Twaha aliwarai wananchi kuungana ili kuhakikisha Bw Odinga anachaguliwa kuwa Rais wa nchi hii ifikapo 2022.

“Raila ni kiongozi ambaye amefungwa jela kwa miaka mingi zaidi akitetea haki za wananchi wa Kenya. Kama njia mojawapo ya kumzawidi, ni vyema tuungane ili kumchagua katika wadhifa huo mkubwa wa Urais nchini,” akasema Bw Twaha.

Mbunge wa Lamu Magharibi, Stanley Muthama aliwarai wananchi kuhakikisha wanampigia kura Bw Odinga ili apate ushindi kwenye uchaguzi ujao wa mwaka 2022.

Viongozi wengine walioandamana na Bw Odinga kwenye ziara hiyo ya siku moja Lamu ni pamoja na Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui, wanasiasa Jeremiah Kioni na Maina Kamanda na aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa zamani wa wanawake Lamu, Shakila Abdalla.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Hadhi ya usomi isidunishwe kwa kutoa vyeti...

MWALIMU WA WIKI: Rashid Kisenya mwalimu dijitali

T L