Makala

LAMU: Sababu 14 kuu zinazowachochea vijana kujiunga na Al-Shabaab zafichuliwa

May 22nd, 2018 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

KUTELEKEZWA kwa kaunti ya Lamu katika masuala ya kimsingi na maendeleo hapa nchini na kubaguliwa kwa wakazi katika kupata haki zao za kimsingi, ikiwemo kumiliki vitambulisho na hatimiliki za ardhi ni mojawapo ya viini vinavyopelekea vijana wengi kujiunga na makundi ya kigaidi eneo hilo.

Wakizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa mpango maalum utakaosaidia kukabiliana na itikadi kali na ugaidi eneo hilo (CVE) Jumanne, wakuu wa usalama, wanachama wa mashirika ya kijamii na wakazi walitaja ukiukaji wa haki za kibinadamu na dhuluma zinazoendelezwa na polisi na jeshi dhidi ya raia pia kuchangia vijana kujiunga na magenge haramu.

Umaskini, ukosefu wa ajira, ufafanuzi finyu wa maandiko ya kidini, mkinzano wa mtazamo wa kisiasa, ukosefu wa elimu, miundomsingi duni, dawa za kulevya na kupotezwa kiholela kwa vijana wakiwa mikononi mwa walinda usalama pia ni miongoni mwa sababu kuu zilizotajwa kuchangia itikadi kali na ugaidi.

Afisa Mkurugenzi wa Kituo cha kushughulikia usaidizi wa kijamii nchini (KEKOSCE), Bi Phyllis Muema (kushoto) na afisa mkuu wa Muhuri, Hassan Abdille wakizungumza na wanahabari mjini Lamu muda mfupi baada ya kuzinduliwa kwa mpango wa kukabiliana na itikadi kali na ugaidi Mei 22, 2018. Picha/ Kalume Kazungu

Mkurugenzi Mkuu wa Kituo kinachojihusisha na usaidizi wa kijamii hapa nchini (KECOSCE), Bi Phyllis Muema aidha aliwataka vijana eneo hilo kuepuka itikadi kali na ugaidi na badala yake kushirikiana vilivyo na serikali na mashirika ya kijamii katika kuafikia Lamu yenye amani.

Bi Muema pia aliitaka serikali ya kitaifa kushirikiana vilivyo na kaunti ili kuona kwamba sababu zinazochangia vijana kujiunga na makundi haramu zinashughukikiwa na ikiwa kuna matatizo yaweze kutatuliwa vilivyo.

Wadau na wakazi wafuatilia kwa makini sababu za vijana kujiunga na makundi ya ugaidi. Picha/ Kalume Kazungu

“Leo tumekutanika hapa Lamu kuzindua vuguvugu litakalosaidia kupigana na itikadi kali na ugaidi. Tumeweza kuibuka na sababu 14 kuu zinazopelekea vijana wa hapa kujiunga na makundi haramu. Ningewasihi wadau wote, ikiwemo serikali kuu, kaunti, viongozi, wanajamii na mashirika yasiyo ya kiserikali kuja pamoja na kushirikiana ili kutatua matatizo yaliyopo na kuhakikisha Lamu inakuwa salama siku zote,” akasema Bi Muema.

Naye Afisa Mkuu wa Shirika la Kutetea Haki za Wailamu nchini (MUHURI), Bw Hassan Abdille, alizitaka serikali za kaunti hasa zile zinazokabiliwa na changamoto ya vijana kujiunga na ugaidi kubuni nafasi za ajira kwa vijana hao.

Wadau walioshirikiana kutayarisha na kuzindua mpango wa kukabiliana na itikadi kali. Jumla ya sababu 14 kuu zinazosukuma vijana wa Lamu kujiunga na Al-Shabaab zilifichuliwa wakati wa kongamano hilo. Picha/ Kalume Kazungu

Bw Abdille pia aliiitaka serikali ya kitaifa kuhakikisha kuna ugavi sawa wa rasilimali kote nchini, ikiwemo Lamu ili kuondoa dhana ya muda mrefu kwamba eneo hilo linabaguliwa katika maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake aidha, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Joseph Kanyiri, alitaja itikadi kali na ugaidi kuwa changamoto ambayo bado inakumba eneo la Lamu.

Aliwataka wakazi kushirikiana vilivyo na vitengo vya usalama ili kukabiliana na ugaidi nchini.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Joseph Kanyiri (kulia) na Kamanda Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Lamu Muchangi Kioi wakati wakifuatilia mazungumzo wakati wa uzinduzi wa mpango wa kukabiliana na itikadi kali na ugaidi Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

“Tatizo la ugaidi na itikadi kali bado ni changamoto hapa Lamu. Kuna baadhi ya vijana wamerudi hapa nchini kutoka Somalia na hawako tayari kujisalimisha kwa idara ya usalama.

Ningeomba familia za vijana kama hao na jamii kwa jumla kuwakabidhi vijana hao kwa idara ya usalama ili wapokee msamaha wa serikali,” akasema Bw Kanyiri.