Habari

LAMU: Wanakijiji wengi Timboni wasema hawajui chochote kuhusu Covid-19

April 29th, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

HUKU serikali na ulimwengu ukiendeleza kampeni kabambe ya vita dhidi ya janga la Covid-19, wakazi wa kijiji cha Timboni, Kaunti ya Lamu hawana ufahamu wowote kuhusu maradhi hayo hatari.

Kijiji cha Timboni ni makazi ya familia zaidi ya 80 ambazo hujishughulisha na kibarua cha kuchimba mawe ili kujipatia riziki ya kila siku.

Kijiji hicho kiko kwenye kisiwa cha Manda, Kaunti ya Lamu.

‘Taifa Leo’ ilipozuru kijiji hicho juma hili, wakazi walionekana kuendeleza shughuli zao kama kawaida bila kuzingata maagizo yoyote ya Wizara ya Afya, ikiwemo kuvaa barakoa, kudhibiti umbali wa mita moja kati ya mtu na mwingine, kuoga au kunawa mikono wakitumia maji safi na sabuni miongoni mwa maelekezo mengine.

Katika mahojiano, wakazi walifichua kuwa hawajapokea ripoti zozote kuhusiana na kuwepo kwa ugonjwa huo hatari kwani hakuna afisa wa serikali au mhudumu yeyote wa afya ambaye amewafikishia ujumbe kuhusiana na kinachoendelea nchini na ulimwenguni.

Kijiji cha Timboni, Kaunti ya Lamu ambapo wakazi hawana ufahamu kuhusu Covid-19. Picha/ Kalume Kazungu

Kijiji cha Timboni hakijafikiwa na stima, hali ambayo imefanya wakazi kuishi bila redio wala televisheni.

Isitoshe, mawimbi ya kupeperusha matangazo ya redio, televisheni na hata simu ni tatizo kubwa eneo hilo.

Hali hii imefanya wakazi kuishi dunia ya zamani isiyokuwa na utandawazi.

Bw Samson Makori alikiri kuona barakoa kwa mara ya kwanza baada ya wanahabari kuzuru eneo hilo juma hili.

Kulingana na Bw Makori, tangu jadi kijiji chao kimekuwa kikitelekezwa kihuduma kutoka kwa serikali, ikiwemo ripoti zinazotolewa kila mara kwa wananchi pamoja na misaada mbalimbali kutokana na kwamba kijiji hicho kinakumbwa na changamoto tele za kimiundomsingi, ikiwemo barabara na mawasiliano.

“Tumeshangaa kwamba nchi yetu inakumbwa na maradhi hatari ya coronavirus ilhali sisi hata taarifa hatuna. Tumeshangaa kuona watu wakivalia vitambaa kwenye pua na midomo. Sisi hatuna ripoti yoyote kuhusu kinachoendelea. Hii ndiyo sababu hata hatujachukua hatua yoyote kujikinga,” akasema Bw Makori.

Bi Mercy Irungu ambaye ni kiongozi wa wanawake katika jamii ya Timboni alisema ni vigumu kwa wanakijiji kuweka umbali wa mita moja kwani mara nyingi wamekuwa wakishirikiana katika mambo mengi, ikiwemo kuchimba mawe kwenye mgodi mmoja katika harakati za kukimu familia zao.

Bi Irungu alisema wakazi pia wamekuwa wakichota maji kijamii kwenye kisima kimoja, hatua ambayo pia inawawia vigumu kuzuia mtagusano.

“Tunahitaji kuelimishwa ili kujikinga dhidi ya Covid-19. Sisi hapa tunalala familia kadhaa kwenye nyumba moja. Pia tunachimba mawe kwa makundi. Isitoshe, hata maji yenyewe ya kutumia tunapata kwenye visima, hivyo lazima tutangamane,” akasema Bi Irungu.

Naye Bw Zablon Barongo alisema ipo haja ya serikali kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma, ikiwemo mawasiliano bila kubagua maeneo ya kufikishwa huduma hizo.

Kwa upande wake aidha, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia alisema hana ripoti yoyote kuhusiana na maeneo ambayo hadi sasa hayajafikiwa na ujumbe kuhusu maradhi ya Covid-19.

Kulingana na Bw Macharia, machifu, manaibu wao na wazee wa mitaa tayari walikuwa wametakiwa kuhakikisha kila eneo linafikiwa na kampeni dhidi ya maradhi ya Covid-19.

“Ninashangaa kwamba kuna sehemu katika ulimwengu huu ambapo wakazi hawana ufahamu kuhusu Covid-19. Hii inamaanisha machifu na wazee wa mitaa kwenye kijiji husika wamezembea kazini. Nitachunguza,” akasema Bw Macharia.