Habari Mseto

Lamu yashangaza kutumia maji ya bahari kukabili corona

April 3rd, 2020 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

MAAFISA wa kitengo cha kukabiliana na majanga wa serikali ya kaunti ya Lamu wamewashangaza wengi pale walipoongoza zoezi la kunyunyiza maji ya chumvi kutoka kwa Bahari Hindi kwa nyumba na maeneo yote ya umma mjini Lamu na viungani mwake kama njia mojawapo ya kukabiliana na janga la corona.

Maafisa hao wakiongozwa na Naibu Afisa Mkuu wa Utawala Katika serikali ya kaunti ya Lamu, Bw Shee Kupi waliunganisha mabomba kutoka sehemu ya Bahari Hindi hadi kwenye maeneo ya nchi kavu kabla ya kuanza shughuli hiyo yak kunyunyizia maji ya chumvi iliyochukua muda wa saa tatu.

Sehemu ambazo zilinyunyiziwa maji hayo ya Bahari Hindi ni mabaraza ambayo wananchi hukaa wakistarehe mbele ya mji wa kale wa Lamu, magati yote ya kushukishia mizigo na abiria mjini Lamu na Mokowe, kuta za nyumba na vioski mbalimbali mjini humo.

Wakazi wa Lamu tangu jadi wanaamini maji ya chumvi kutoka kwa Bahari Hindi yana uwezo wa kuua virusi, vimelea na kutibu magonjwa mengi.

Bw Kupi alisema shughuli hiyo ambayo ni ya awamu ya kwanza itakuwa ikitekelezwa kila baada ya wiki moja na kwamba vijiji vyote vya Lamu pia vitakuwa vikipuliziwa maji hayo.

Wakazi wa Lamu wanaamini maji ya chumvi kutoka baharini yana uwezo wa kukabiliana na maradhi na kuua virusi. Picha/ Kalume Kazungu

Alisema wataendelea kutekeleza shughuli hiyo ya kunyunyiza maji ya chumvi wakati wakisubiri serikali kupitia kwa Wizara ya Afya nchini kuwaletea dawa maalum zitakazotumika kunyunyiza miji na hewa kama inavyofanyika jijini Nairobi.

Bw Kupi aliwataka wakazi kushirikiana kikamilifu katika kuhakikisha zoezi hilo la kunyunyiza maji ya Bahari kwenye mabaraza ya umma na yale ya kibinafsi linafaulu kila litakapokuwa likiandaliwa.

“Kuna wale ambao bila shaka wanashangaa iweje maji ya Bahari Hindi kutibu coronavirus? Watambue kuwa haya maji ni ya chumvi na tangu jadi hapa Lamu wazee wetu wamekuwa wakiyatumia kama tiba ya maradhi tofauti tofauti.

“Sisi nasi tumeafikia kutumia maji hayo kunyunyiza mabaraza yetu, kuta na hata sehemu zote zinazotumiwa na umma ili kujaribu kusaidia kukabiliana na hili janga la Covid-19. Tunaamini kabisa kwamba virusi vya corona vikiwa kwenye mazingira yetu vitamalizwa na haya maji ya chumvi kutoka baharini,” akasema Bw Kupi.

Shughuli hiyo aidha ilipokelewa vyema na baadhi ya wakazi wa Lamu ilhali wengine wakiikashifu.

Bw Mohammed Ali ambaye ni mzee a Lamu alitaja hatua hiyo kuwa ya busara, akisisitiza kuwa maji ya chumvi kutoka baharini ni tiba ya maradhi, ikiwemo kuua virusi vya corona.

Mafisa wa kitengo cha kukabiliana na majanga kaunti ya Lamu wakiendeleza shughuli ya kunyunyiza maji ya chumvi kutoka kwa bahari hindi mitaani, mabarazani na kwenye majumba katika harakati za kukabiliana na virusi vya corona. Picha/ Kalume Kazungu

“Tunashukuru kaunti yetu kwa jitihada zake katika kukabiliana na janga la Corona. Hatua waliyochukua ya kuosha mabaraza yetu na sehemu zetu za umma kwa maji ya chumvi kutoka baharini ni ya busara. Virusi vingi havina nguvu ya kuishi kwenye mazingira ya chumvi. Zoezi liendelee. Tunaliunga mkono mia fil mia,” akasema Bw Ali.

Naye Ahmed Omar alikashifu hatua hiyo akidai ni ukosefu wa uwajibikaji kwa serikali ya kaunti ya Lamu.

Alisema wananchi wamejionea kaunti kama vile Nairobi zikisambaza magari ya kunyunyiza dawa za kukabiliana na virusi vya Corona kwenye mitaa, barabara, mabaraza na sehemu zote za umma.

“Serikali za kaunti, ikiwemo Lamu ziko na fedha za kutosha kukabiliana na majanga. Kwa nini wasitumie fedha hizo kununua dawa zilizopasishwa na wanasayansi ili kukabiliana na virusi vya Corona? Kupuliza maji ya chumvi mabarazani na sehemu za umma huko ni kuzembea na pia ni mbinu ya kutafuta jinsi watakavyofuja fedha zilizopangiwa zoezi hilo la kunyunyiza dawa mitaani kwa minajili ya kukabiliana na Coronavirus,” akasema Bw Omar.