Habari Mseto

Lamu yatenga mamilioni kusajili wakazi kwa bima ya NHIF

May 26th, 2018 1 min read

Na KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya Kaunti ya Lamu imetenga jumla ya Sh120 milioni kwenye bajeti iliyopitishwa na Bunge la kaunti hiyo juma hili ili kusajili familia 20,000 katika mpango wa Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF).

Awali, Gavana wa Lamu, Fahim Twaha alikuwa ameahidi kwamba utawala wake utahakikisha kila mkazi wa Lamu ananufaika na mpango huo wa NHIF.

Katika bajeti hiyo ya jumla ya Sh 4.5 bilioni ya mwaka wa kifedha wa 2018/2019, Sh 200 milioni zilitengewa mradi wa kununua na kuweka taa za barabarani kote Lamu.

Mgao mwingine wa Sh 123 milioni ulitengwa kwa minajili ya kuunganisha mifereji na mabomba ya kupitisha maji hadi kwenye maeneo ya vijijini ilhali Sh 78 milioni nyingine zikitengewa masomo ya shule za chekechea (ECDE).

Bunge la Kaunti ya Lamu limepitisha bajeti ya Sh 4.5 bilioni ya mwaka wa kifedha wa 2018/2019 ambapo Sh120 milioni zilitengewa usajili wa familia 20,000 za Lamu katika mpango wa bima ya kitaifa ya afya (NHIF). Picha/ Kalume Kazungu

Sh 50 milioni pia zilitengwa kwenye bajeti hiyo ili kuweka lami katika maeneo ya miji (cabro) ilhali Sh 30 milioni zikitengewa ununuzi wa mbegu na pembejeo ili kuimarisha kilimo eneo hilo.

Mgao mwingine wa Sh 15 milioni ulitengewa usajili wa vijana katika mafunzo ya kuendesha magari na boti na kuhakikisha wamepata leseni za kuendeshea vyombo hivyo.

Hoja ya kupitisha bajeti hiyo iliwasilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti, Bw Azhar Mbarak, ambapo wawakilishi wa wadi kwenye bunge la Lamu waliipokea na kuipitisha kwa kauli moja.

Akizungumza muda mfupi baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Mwakilishi wa Wadi ya Hongwe, James Komu, alisema amefurahia bajeti hiyo kutokana na kwamba imeweka kipaumbele masuala ya maendeleo ya kaunti.

“Nimefurahishwa sana na bajeti tuliyopitisha. Tulipigania kuona kwamba sekta ya maendeleo inapata mgao wa hadi asilimia 42 ya bajeti yote. Safari hii pia kila diwani bungeni ameruhusiwa kutoa maoni yake kinyume na ilivyokuwa awali ambapo kupitisha bajeti kama hii ilikuwa msukumano,” akasema Bw Komu.