Makala

Larry Mutunga: Anatumai kuwika katika soka, alenga kuiga Sergio Busquets

May 21st, 2019 3 min read

Na PATRICK KILAVUKA

UNAPONUIA kufanya jambo litekeleze kwa moyo na kujituma ili uyaafikia malengo yako.

Huo ndiyo ushauri wa mwanasoka Larry Mutunga mwenye umri wa miaka 22.

Akiwa kinda mwanasoka Mutunga alikuwa anawazia kuwa mwanasoka mahiri siku za usoni.

Jambo hilo lilikuwa linapita akilini mwake kila uchao.

Kama ndoto ya kweli ambayo inaelekea kutimia, anakumbuka kuanza kujitosa uwanjani akiwa darasa la kwanza Shule ya Msingi ya Esibembe, Maseno na anaendelea kutia bidii ya mchwa ambayo imempelekea  kuzichezea timu mbalimbali za mitaani katika Ligi na chuo anakosomea.

Mwanasoka Larry Mutunga akitoka uwanjani baada ya mchezo kutamatika baina ya timu yake dhidi ya Chuo cha Cooperative katika uga wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN). Picha/ Patrick Kilavuka

Japo mwanasoka Mutunga anacheza kama kiungo mvamizi, alianza kucheza kama fowadi akiwa shule ya msingi ambayo iilitajwa kabla kuendeleza ubabe wake wa soka katika Shule ya Upili ya Emusire High na kuchezeshwa nafasi ya kiungo cha kati na kuboresha matokeo ya mchezo shuleni na kuifanya shule yake kufanya vyema katika mashindano.

“Niliaminiwa na kocha wa shule safu hiyo kwani alisema anatamani kuona nikijijenga zaidi kuinuia kiwango cha mchezo wangu mbali na kuleta nguvu mpya katika safu ya mashambulizi pia,” anasema Mutunga ambaye akiwa katika darasa la sita, alipata nafasi ya kuchezea timu ya mtaani ya Maseno United chini ya kocha wake Fredrick Khagali aliyemwamini kucheza safu ya fowadi kikosini mwake.

Mwaka wa 2014, huduma zake zilihemewa sana na timu hiyo wakati walikuwa wanacheza Ligi ya kaunti ndogo ya Maseno na kuiwezesha timu ya United kutamba katika ligi hiyo.

Kweli chema chajiuza.

Mwaka 2017 alisajiliwa na Academy ya Impala na kuicheza katika kipute cha Afrika Mashariki.

Weledi wake katika soka ulitambuliwa baada kutawazwa mchezaji bora katika dimba hilo ambalo liliandaliwa Impala hapa nchini.

Mwaka uo huo (2017) nyota yake ya jaha ilizidi kung’aa pale ambapo alishirikishwa katika kikosi ambacho kilicheza michuano ya Ligi ya Shirikisho la Kandanda Nchini (FKF), tawi la Nairobi West na akaifungia magoli mawili akicheza kama beki mtambaji au kiungo mvamizi. Alimega pia pasi za uhakika ambazo zilisababisha magoli pia.

Kabla ajiunge na timu ya Chuo cha Strathmore mwezi wa Novemba ambako anasomea taaluma ya Tekinolojia na Mawasiliano, alikuwa ameisakatia timu yake ya Imapla Ligi ya FKF, Kaunti, tawi la Nairobi West na kuisaidia katika upachikaji wa mabao.

Kwa vile chanda chema huvikwa pete, mwanakabumbu huyo alipojijunga na chuo hiki ambacho kilikuwa kimefuzu Ligi ya Daraja ya Kwanza mwaka huu, alipatia fursa ya moja kwa moja kwani mkufunzi wake Mike Weche (aliyekuwa kigogo wa zamani wa Ingwe) anasema hakuona lengine la kufanya kwani, baada tu kukanyaga tu guu lake la dhahabu uwanja kwa mara ya kwanza na kuona vile alivyokuwa akifanya mazoezi yake, moyo wake  ulitulia kwa sababu aliona kifaa cha kudhibiti safu ya  kati katika kikosi chake kwani, nafasi hiyo ilikuwa inamkosesha usingizi katika kumsakasaka kiungo ambaye anaweza kumwajibisha safu hiyo katika timuni kusukuma guruidumu la ligi hiyo.

“Kutoka tu siku ya kwanza ya kujinoa, niliona utajiri mkubwa wa kipaji cha soka kwani alikuwa mwepesi wa kufuata ushauri, kufanya mazoezi kwa kujituma, kupiga pasi za uhakika, chenga maridhawa na alikuwa anauchukua mpira kwa urahisi kutoka kwa mpinzani. Isitoshe, ni msakataji soka ninayeweza kumtumia kucheza katika kila idara muhimu kikosini iwapo kuna majeruhi,” anadokeza kocha Mike  ambaye alikuwa  beki stadi wa jadi zama zake akipepetea kambi ya AFC Leopards.

Sifa

Mchezaji mwenzake George Makau anamsifu mwanadimba huyo kutokana na uhusiano wake wa rahisi na wachezaji wenza timuni kwa kipindi kifupi ambacho alisajiliwa na timu na amekuwa kiungo wa kutegemewa sana tangu mwishomwisho mwa mwaka 2018.

Mutunga anasema kucheza michuano ya daraja za juu kwake ni kama kigezo cha kuimarisha uchezaji wake  licha ya kwamba anapitia changamoto kadhaa kutoka kwa wanasoka wenye uzoefu mwingi

“Wakati mwingi unachezewa tu sivyo baada ya kumlisha mtu kanzu, chenga ya kishua au kumpita na kumuacha ameduwaa kisha anaibika na wakati unashika boli, yeye hutegea tu kukuchezea ngware,” anakiri mwanakandanda huyo ambaye ana kila sabubu ya kusema kwamba ana matumaini tele ya kupiga gozi hadi daraja la juu nchini na hata kuzidisha kiu ya kucheza ughaibuni.

Anaongezea kuwa, kuyapitia mapito kama hayo, kwake ni kama ngazi pia ya ufanisi kwani anaamini katika kila jambo, kikuu ni kusimama kidete katika unalokusudia mbeleni au usoni na kuyasahau yaliyopita kwa kuganga yajayo kitaaluma au kitalanta.

Mwanasoka Mutunga angependa kufanya mazoezi kwa bidii sana na kutazama jinsi vile wachezaji wengine wanasakata kabumbu huku akizamia kuvalia jezi ya kiungo Sergio Busquets wa Barcelona na Mkenya Victor Wanyama ambaye anaichezea Tottenham Hotspurs.

Mipango ya mchezaji huyu ni kusawazisha masomo na talanta ili kujikuza zaidi katika nyanja zote akilenga kuchezea timu kubwa katika Ligi Kuu Kenya na Ughaibuni.

Hapa nyumbani angependa kuichezea Gor Mahia na ughaibuni bila shaka analenga kuichezea Manchester United.