Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALLAH: Jogoo mwoga aghalabu huwa ndiye mfalme

December 23rd, 2020 2 min read

NA WALLAH BIN WALLAH

WAHENGA walisema kwa mwoga huenda kicheko kwa shujaa huenda kilio. Ukweli ni kwamba waoga hufa mara nyingi sana maishani kabla hawajafa kifo cha kweli!

Lakini wanaishi miaka mingi zaidi kabla hawajafa kweli! Shujaa hufa mara moja tu! Kifo cha shujaa hutokea haraka zaidi ndiyo maana mashujaa hawana maisha marefu. Kinachobakia cha kujivunia kwa shujaa ni kwamba huwa amekufa kishujaa! Lakini kifo ni kifo tu, hakuna kifo kitamu!

Licha ya hayo, ni bora kuwa mwoga, mpole na mnyenyekevu wa kupiga magoti chini kuliko kujitutumua na kujipiga kifua wakati mambo yanapokuwa moto!

Heri uwe kama nyasi usipigane na moto mkali nyikani. Tafadhali, okoa roho yako moja aliyokupa Mwenyezi Mungu kwa kuitunza vizuri isikutoke! Bora kuwa mwoga uishi kuliko kuwa shujaa uishe!Katika kijiji cha Kukupunda walikuwapo jogoo wawili waliopigania ufalme wa kutawala kijiji cha Kukupunda.

Kila jogoo alitaka kuwa mfalme wa kuwatawala kuku pamoja na vifaranga pale kijijini Kukupunda. Vita vikatokea kati ya Jogoo Mwekundu na Jogoo Kijivu! Vilikuwa vita vikali vya kuogofya! Jogoo Kijivu na Jogoo Mwekundu walipapurana kwa kucha na kudonoana kwa vidona vyao kwa hasira na hamaki!

Kuku wengine na vifaranga walitazama kwa wasiwasi kisirisiri tu!Jogoo Mwekundu ndiye aliyeonyesha ujeuri na ubabe zaidi. Jogoo Kijivu alimwambia Jogoo Mwekundu, ‘Tusipigane bure! Tutaumizana bure! Vita ni hasara, havina faida! Tusipigane!’

Hapo ndipo Jogoo Mwekundu alipochachamaa na kujipiga kifua zaidi akaongeza hasira kumshambulia Jogoo Kijivu! Akamparuza na kumdonoadonoa kichwani, machoni na kwenye undu!

Jogoo Kijivu akavuja damu kichwani! Aliogopa akakimbia kuingia katika nyumba kujificha chini ya kitanda! Jogoo Mwekundu alipoona mwenzake amekimbia, alijipapatua mbawa zake akawika kwa maringo kutangaza ushindi, ‘Mimi ndiye mfalme wa kuku wote kijijini Kukupunda!’

Alitaka dunia nzima ijue kwamba alishinda. Akapanda juu kabisa kwenye paa la nyumba akawika kwa nguvu, ‘Kokoikoooo!!! Nimeshindaaaa!! Mimi mfalme wenu kuanzia sasa hivi!!’

Jogoo Mwekundu alipokuwa kwenye paa akijisifu na kujitangazia ufalme, tai mkubwa aliyekuwa kwenye mti mbali mlimani, alikuja upesi kama umeme akamnyakua chwap!!! Akaenda naye kwa watoto wake kiotani wakamla Jogoo Mwekundu bila ya kujitetea!

Yule Jogoo Kijivu mwoga alitokeza polepole akatangazwa rasmi bila wasiwasi kuwa ndiye mfalme wa Kukupunda mpaka leo!Ndugu wapenzi, piga magoti usipige kifua! Waoga hufa mara nyingi, lakini wanaishi miaka mingi duniani. Jogoo mwoga ndiye hutokea kuwa mfalme!

Kwa mwoga huenda kicheko! Kuwa mnyenyekevu katika dunia hii ya Mungu!!!!!