Habari MsetoVideo

Lazima KANU iwe debeni 2022 – Nick Salat

June 15th, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KATIBU Mkuu wa Kanu Nick Salat ametangaza kuwa chama Kanu kimeanza mazungumzo na vyama mbalimbali vya kisiasa kama hatua ya kujiandaa kwa uchaguzi mkuu  wa mwaka wa 2022.

Akiongea katika makao makuu ya chama hicho Jumatano jioni, Bw Salat alisema mazungumzo hayo yanashirikisha wanasiasa kutoka vyama mbalimbali vikiwemo Wiper, ODM, ANC, Ford Kenya na baadhi ya wanasiasa walioko ndani ya chama cha tawala cha Jubilee.

“KANU itashiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022 ndiposa tumeanzisha mazungumzo na vyama vingine kwa lengo la kuhakikisha kuwa tunafikia lengo hilo. Hii ndio maana Kanu haitaki kushiriki katika ushindani wa kisiasa wakati huu kwani hatua hiyo inaweza kuvuruga mipango yetu,” akaeleza Bw Salat

Hata hivyo, Bw Salat hakufafanua ikiwa mwenyekiti wa Kanu Seneta Gideon Moi atashiriki uchaguzi huo au ataunga mkono mgombeaji wa urais kutoka chama kingine.

“Kile mnapaswa kujua ni kwamba Kanu itakuwa mhusika mkuu katika uchaguzi wa urais mwaka wa 2022. Ni hiyo ndio mojawapo ya sababu zilizotuchangia hatua yetu ya kuwadhamini mgombeaji katika uchaguzi mdogo wa kiti cha eneo bunge la Baringo Kusini,” akasema.

Chama hicho kilitangaza kuwa kitamuunga mkono mgombeaji wa Jubilee Bw Charles Kamuren ambaye alikuwa mgombeaji wake katika chaguzi mbili zilizopita za miaka ya 2007 na 2013.

Hivi majuzi Bw Moi alisema kwamba atafanyakazi pamoja na  Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022. Alisema hayo alipomtembelea gavana huyo ambaye ni naibu kiongozi wa ODM, afisini mwake mjini Mombasa wiki moja iliyopita.

Na mapema wiki hii chama cha Wiper kiliungama kuwa chama cha Kanu ni mojawapo ya vyama ambavyo kinafanya mazungumzo navyo kwa lengo la kubuni muungano wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu uliopita.

Video Gallery