Siasa

Lazima niwanie urais 2022 – Kalonzo

September 14th, 2020 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, amesisitiza kuwa atawania urais mnamo 2022 licha ya chama chake kuwa kwenye mkataba wa kisiasa na Chama cha Jubilee (JP).

Bw Musyoka alitoa tangazo hilo jana baada kukamilika kwa kikao cha siku mbili cha Baraza Kuu la Chama kwenye hoteli moja, Kaunti ya Machakos.

Huenda kauli ya Bw Musyoka ikazua hali ya suitafahamu, hasa baada ya chama chake kutia saini mkataba wa ushirikiano na JP mnamo Juni.

Mkataba huo pia ulitiwa saini na vyama vya Kanu na Chama cha Mashinani (CCM).Bw Musyoka alisema kwamba tayari, chama kimeanza harakati za kujitayarisha kwa uchaguzi huo, kwa kuweka mfumo wa kidijitali kwenye usajili wa wanachama wake.

“Tumeimarisha mfumo wa usajili wa wanachama wapya tukiwalenga vijana, kwani ndio wengi nchini,” akasema.

Tangazo la Bw Musyoka pia linatarajiwa kuongeza ushindani wa kisiasa katika eneo la Ukambani, hasa baada ya baadhi ya viongozi kuanza kumpigia debe Naibu Rais William Ruto, wakiongozwa na aliyekuwa Seneta wa Machakos, Johnstone Muthama.

Wiki mbili zilizopita, Dkt Ruto alizuru katika eneo la Athi River na kuwarai wenyeji kuunga mkono azma yake. Magavana Alfred Mutua (Machakos) na Kivutha Kibwana (Makueni) pia wametangaza azma zao kuwania urais kwenye uchaguzi huo.

Licha ya tangazo hilo, Bw Musyoka alisema chama hicho kinaunga mkono kikamilifu Mpango wa Maridhiano (BBI) na kitashiriki kwenye kampeni za kuupigia debe.

“Wiper itazuru kila sehemu nchini kuipigia debe BBI kwa kuwashirikisha wananchi. Tunaona hitaji kuu la mpango huo, hasa wakati huu ambapo baadhi ya viongozi wameanza kueneza taharuki za kisiasa. Tunaunga mkono mpango wa Rais Uhuru Kenyatta kuacha nchi yenye msingi thabiti kisiasa,” akasema.

Bw Musyoka pia alikosoa taswira inayosawiriwa kwenye mpango huo kama ushindani wa kisiasa kati ya Dkt Ruto na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Wawili hao wamekuwa wakielekezeana lawama za kisiasa, Dkt Ruto akishikilia kuwa lazima mageuzi yoyote ya kikatiba yakitwe kwenye maslahi ya wananchi, lakini si kuwatengenezea viongozi nyadhifa za kisiasa.

Hata hivyo, Bw Odinga amekuwa akisisitiza mpango huo utakuwa njia mwafaka ya kuondoa migawanyiko ambayo imekuwa ikishuhudiwa nchini.

Chama pia kilipinga pendekezo la kubuniwa kwa serikali za kikanda, badala yake kikisema Serikali ya Kitaifa inapaswa kuweka mikakati kuimarisha mfumo wa ugatuzi.Kilitaja kubuniwa kwa Hazina ya Kuzistawisha Wadi kama njia mwafaka zaidi ya kuimarisha mfumo huo.