HabariSiasa

Lazima Ruto aingie Ikulu – Tangatanga

September 2nd, 2019 1 min read

Na GEORGE MUNENE

WABUNGE 18 kutoka eneo la Mlima Kenya wanaoegemea mrengo wa Tangatanga Jumapili walisisitiza kuwa Naibu wa Rais William Ruto ndiye atakayemrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022.

Wabunge hao pia walipuuzilia mbali Kamati iliyobuniwa na Rais Kenyatta pamoja na kiongozi wa ODM Raila Odinga kukusanya maoni kuhusu namna ya kuunganisha Wakenya, maarufu BBI.

Wanasiasa hao walisema kuwa Naibu wa Rais Dkt ruto hatalegeza kamba katika mbio zake za kuelekea Ikulu 2022.

Wakizungumza katika Shule ya Msingi ya Kangaita, Kaunti ya Kirinyaga, wabunge hao walimtaka Bw Odinga kuzika ndoto yake ya kutaka kuongoza Kenya katika kaburi la sahau.

Walimhakikishia Dkt Ruto kuwa eneo la Mlima Kenya litamuunga mkono katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Wabunge hao walijumuisha Munene Wambugu (Kirinyaga ya Kati), Gichimu Githinji (Gichugu), George Kariuki (Ndia), Rigathi Gachagua (Mathira), Gitonga Murugara ( Tharaka),Ndindi Nyoro (Kiharu), Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Jane Kihara (Naivasha), Gichunge Kabeabea (Tigania Mashariki), Michael Muchira (Olojorok), Mary Wamahua (Maragwa) na Benjamin Mwangi ( Embakasi ya Kati)

Wengine ni Wawakilishi wa Wanawake Wangui Ngirici (Kirinyaga), Beatrice Nkatha (Tharaka Nithi) na Faith Gitau (Nyandarua).

Wabunge hao waliokuwa wameandamana na Dkt Ruto walisema kuwa jopokazi la BBI linalenga kumwezesha Bw Odinga kuwa rais 2022.

“Jopokazi la BBI linalenga kuhakikisha kuwa Dkt Ruto haimrithi Rais Kenyatta 2022,” akasema Bw Wambugu.

Bi Ngirici alitaka jopokazi la BBI kuvunjiliwa mbali huku akisema linaharibu fedha za walipa ushuru bure.