Michezo

Lazima tujipange kabla ya mechi za marudiano – Odera

August 6th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Paul Odera amekiri kuna kazi kubwa ya kufanywa kabla ya Simbas kualika Zambia (Agosti 24) na mabingwa watetezi Zimbabwe (Septemba 21) katika mechi za marudiano za raga ya wachezaji 15 kila upande ya Victoria Cup.

Akizungumza na Taifa Leo baada ya Simbas kuzimwa 30-29 na Zimbabwe mjini Bulawayo, Odera alisema, “Ilikuwa mechi ngumu jinsi nilivyobashiri itakuwa. Tumejifunza jinsi ya kukabiliana na mashambulizi na kulinda ngome yetu pembeni. Hata hivyo, kazi bado ipo kabla ya mechi ya marudiano.”

Kabla ya kucheza na Zimbabwe hapo Agosti 3, Odera alikuwa ametabiri kuwa mechi dhidi ya wapinzani hawa itakuwa kali zaidi katika mashindano haya ya mataifa manne.

“Mechi dhidi ya Zimbabwe itakuwa ngumu kabisa. Motisha yetu iko juu. Wachezaji wazoefu wanashirikiana vyema na wale chipukizi kwa karibu. Tunathamini ujuzi wa wachezaji waliowahi kucheza kombe hili mjini Bulawayo,” alisema Odera kabla ya mechi hiyo ambayo Kenya ilipata alama zake kupitia kwa Monate Akuei (miguso miwili), Anthony Odhiambo (mguso mmoja na mkwaju), Elkeans Musonye (mguso mmoja), Johnstone Mung’au (mguso mmoja) na Charles Kuka (mkwaju).

Nahodha wa Zimbabwe, Hilton Mudariki alifungia timu yake alama 15 nao Takudzwa Kumadiro, David Makanda na Biselele Tshamala wakachangia mguso mmoja kila mmoja.

Kichapo hicho kilikuwa cha kwanza cha Kenya dhidi ya Zimbabwe tangu ilimwe 28-20 uwanjani Prince Edward mwaka 2015.

Tangu wakati huo, Kenya ilikuwa imetawala michuano yake dhidi ya Zimbabwe ikiwemo kubwaga Wazimbabwe mara mbili nchini Zimbabwe na moja jijini Nairobi.

Simbas iliingia nchini Zimbabwe ikitokea Zambia ambako ilikuwa imetamba 43-23 mjini Kitwe.

Majeraha ziarani

Ziara za Kenya nchini Zambia na Zimbabwe zilishuhudia ikipata majeraha matatu.

Isaac Njoroge alipata jeraha la kichwa dhidi ya Zambia mnamo Julai 27.

Hakushiriki mechi ya Zimbabwe baada ya kufeli uchunguzi wa kimatibabu.

Patrick Ouko na Melvin Thairu walipata majeraha ya kifundo dhidi ya Zimbabwe.

Baada ya mechi za wikendi, Zimbabwe inaongoza jedwali la Victoria Cup kwa alama 15.

Iliingia mechi ya Kenya na motisha ya kupepeta Zambia 39-10 (Julai 13) na Uganda 31-26 (Julai 27).

Kenya ni ya pili kwa alama 11 baada ya kupoteza pembamba dhidi ya Zimbabwe na kulima Uganda 16-5 na Zambia 43-23.

Uganda ina alama mbili kwa kupoteza pembamba dhidi ya Zimbabwe. Aidha, mechi kati ya Uganda na Zambia iiliyoratibiwa kusakatwa Agosti 10, imeahirishwa hadi Agosti 17.

Mabadiliko haya, kwa mujibu wa Shirikisho la Raga nchini Uganda, yalifanywa baada ya Zambia kuomba mchuano huo usukumwe mbele kutokana na mabadiliko katika mipango ya usafiri. Simbas ilirejea nchini Jumapili jioni.