Michezo

Lazima Zoo Kericho initambue, aapa Alwanga

August 24th, 2018 1 min read

NA CECIL ODONGO

MSHAMBULIZI wa Mabingwa wa KPL mwaka wa 2008 Mathare United Clifford Alwanga ameahidi kutokomeza ukame wa magoli unaomkumba kwa kutikisa nyavu za Zoo Kericho katika mechi yao Jumamosi  Agosti 25 ugani Kericho Green Stadium.

Zana za Alwanga ambaye ni mfungaji bora wa Mathare zimekuwa butu langoni mwa washindani wao huku ukame wa kutotikisa nyavu ukimkumba katika mechi nane zilizopita.

Mikosi ya kupoteza penalti pia zimemwandama straika huyo kwa kuwa amepoteza penalti mbili, ya hivi majuzi ikiwa katika mechi dhidi ya Nakumatt FC ambapo walipokezwa kichapo kizito cha 4-0, Jumamosi Agosti 18.

“Ni masikitiko kwamba sijakuwa na bahati ya kuyafuma magoli ingawa nimekuwa nikijituma sana. Nimeyafunga mabao matano dhidi ya Zoo na hilo linanipa imani ya kutikisa nyavu zao,” akasema Alwanga ambaye amewafungia Mathare mabao kumi msimu huu katika mashindano mbalimbali.

Aidha sogora huyo alifichua kwamba alitazama mechi kati ya Zoo FC na mabingwa mara 11 wa KPL, Tusker iliyosakatwa Agosti 19 ugani Ruaraka na akafahamu udhaifu wa wapinzani utakaomwezesha kutamba katika mechi ya Jumamosi.

Mathare United wanaoshikilia nafasi ya saba kwa alama 38 katika msimamo wa jedwali la ligi watalazimika kucheza kwa tahadhari dhidi ya Zoo ambao wanalenga kuepuka shoka ya kuteremsha ngazi mwisho wa msimu huu