Michezo

Lazio wasajili 'nyani' mkongwe Pepe Reina

August 29th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

LAZIO wamejinasia huduma za kipa mkongwe mzawa wa Uhispania, Pepe Reina, 38, kwa mkataba wa miaka miwili.

Hii ni baada ya mlinda-lango huyo wa zamani wa Liverpool kuagana rasmi na AC Milan ambao ni washindani wakuu wa Lazio katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Reina aliwajibishwa na Uhispania katika jumla ya mechi 36 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichonyanyulia Uhispania ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2010 nchini Afrika Kusini.

Reina alichezea kikosi cha Aston Villa msimu huu wa 2019-20 kwa mkopo kutoka Juventus na akawasaidia kukwepa shoka la kuwashusha ngazi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) chupuchupu.

Ingawa matamanio makubwa ya Reina ni kunogesha kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), huenda Lazio wakamwajibisha zaidi kwenye Ligi Kuu na mapambano ya Coppa Italia kwa kuwa atakuwa kipa chaguo la pili nyuma ya mlinda-lango mzawa wa Albania, Thomas Strakosha, 25.

“Reina ni miongoni mwa makipa mahiri zaidi katika historia ya soka na anatua Lazio akijivunia tajriba pana itakayotutambisha zaidi kwenye kampeni zijazo,” ikasema sehemu ya taarifa ya Lazio.

Lazio walikamilisha kampeni za Serie A msimu huu wa 2019-20 katika nafasi ya nne na wakafuzu kwa kipute cha UEFA kwa mara ya kwanza baada ya kuwa nje kwa kipindi cha miaka 13.

Reina alitua ugani San Siro kuvalia jezi za AC Milna mnamo Julai 2018 baada ya kuagana rasmi na Napoli. Hata hivyo, alichezea Milan katika jumla ya mechi 13 pekee kabla ya kutumwa Villa kwa mkopo mnamo Januari 2020.

Aliwajibishwa na Liverpool Uingereza katika jumla ya mechi 398 baada ya kusajiliwa kutoka Villarreal ya Uhispania mnamo 2005. Alihamia Bayern Munich ya Ujerumani mnamo 2014 kabla ya kuyoyomea Italia kuvalia jezi za Napoli kwa kipindi cha misimu mitatu.