Habari Mseto

Leba Dei: Wafanyakazi waitaka bunge kupuuza mageuzi ya sheria za leba

May 1st, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

VIONGOZI wa vyama vya wafanyakazi na waajiri, Jumanne walitumia sherehe za Leba Dei za mwaka huu kuitaka serikali kusitisha mabadiliko ya sheria za Leba.

Wakihutubu katika bustani ya Uhuru Park ambako sherehe hizo ziliandaliwa, viongozi hao walisisitiza kuwa mabadiliko hayo yananuiwa kunyima wafanyakazi haki zao za kikatiba na hawatayakubali.

“Wafanyakazi wamekataa mabadiliko yoyote ya kisheria ambayo yanalenga kuwanyima haki zao za kikatiba. Tunasema kwamba hatutakubali,” alisema Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (Cotu) Bw Francis Atwoli.

Aliwataka wabunge kukataa mabadiliko hayo yakiwasilishwa mbele yao. “Tunataka uhusiano mzuri ili kuimarisha mazingira ya kufanyakazi nchini na sio kubadilisha sheria,” alisema

Katibu Mkuu wa chama cha walimu nchini Wilson Sossion alisema wafanyakazi hawatakubali wawakilishi wao kuondolewa katika bodi ya wasimamizi wa ya Shirika la Malipo ya Uzeeni (NSSF).

“NSSF ni la wafanyakazi. Ni hazina ya wafanyakazi na hatutakubali wawakilishi wa Cotu waondolewe kupitia mabadiliko ya sheria,” alisema. Akipinga mabadiliko hayo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Waajiri Kenya (FKE) Bi Jackline Mugo alisema mashauriano yanahitajika kati ya washikadau wote.

“Mabadiliko hayo yanafaa kusimamishwa kwa sababu hayawakilishi maslahi ya wafanyakazi,” alisema.

Bw Atwoli alisema wafanyakazi hawatakubali ufisadi katika NSSF. Kwenye hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Leba Ukur Yattani, Rais Kenyatta alisema mageuzi ya kisheria ni muhimu ili kuhakikisha shirika hilo linasimamiwa vyema.