Habari

Leba Dei ya malumbano kati ya COTU, NHIF na NSSF

April 30th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wanaadhimisha siku ya wafanyakazi ulimwenguni Jumanne huku vyama vya wafanyakazi na serikali vikizozana kuhusu mabadiliko ya sheria yanayolenga kuondoa wawakilishi wao katika mashirika mawili yanayohifadhi mabilioni ya pesa zao.

Maafisa wa vyama vya wafanyakazi nchini wanapinga mabadiliko ya sheria yanayolenga kuondoa wawakilishi wa wafanyakazi katika bodi za Shirika la Taifa la Malipo ya Uzeeni (NSSF) na Shirika la Bima la Taifa la Afya (NHIF).

Wafanyakazi huchanga mabilioni ya pesa katika mashirika haya na muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini (Cotu) huwakilisha maslahi yao katika bodi za kuyasimamia.

Hata hivyo, Wizara ya Leba inapendekeza sheria ibadilishwe ili wawakilishi wa wafanyakazi waondolewe katika bodi hizo. Katibu Mkuu wa Cotu Francis Atwoli na Katibu Mkuu wa chama cha walimu nchini Wilson Sossion wamepinga mapendekezo hayo wakisema mabadiliko hayo siyo ya kikatiba.

“Tuko tayari kupinga mabadiliko yaliyopendekezwa kortini kwa sababu yote yanaonekana kulenga haki za kikatiba za wafanyakazi. Baadhi ya watu wanataka kutumia sheria kunyima Wakenya haki zao za kikatiba,” alieleza Bw Sossion.

Miongoni mwa mabadiliko yanayopendekezwa ni wafanyakazi wanaonuia kugoma kutoa notisi ya siku 21 badala ya saba ilivyo kwa wakati huu.

Yakipitishwa na bunge, wafanyakazi hawatakuwa wakipeleka mizozo mahakamani moja kwa moja kabla ya kujaribu mbinu tofauti za upatanishi. Kulingana na waziri wa Leba Ukur Yattani, pendekezo hili linalenga kutatua mizozo ya wafanyakazi kabla ya kufika kortini na kulemaza huduma.

Vyama vya wafanyakazi vinahisi kwamba serikali inataka kuwa na idadi kubwa ya wawakilishi katika bodi ya NSSF ili kuwa na usemi mkubwa kuhusu pesa za wafanyakazi. “NSSF ni shirika la wafanyakazi na hawawezi kunyimwa nafasi ya kuwa na usemi kuhusu mali yao,” asema Bw Atwoli.

Lakini Bw Yattani anatofautiana nao akisema wameshindwa kuhakikisha shirika hilo linasimamiwa vyema.

“Kuna mipango duni ya uwekezaji katika NSS, usimamizi mbaya na ufisadi wa hali ya juu. Dhana kwamba washikadau ndio wasimamizi bora ni la kupotosha lau sivyo, NSSF lingekuwa limesimamiwa vyema kwa sababu Cotu na Shirikisho la Waajiri (FKE) zimewakilishwa,” alisema waziri Yattani.