Leeds United wanyima Liverpool fursa ya kutinga ndani ya mduara wa nne-bora EPL

Leeds United wanyima Liverpool fursa ya kutinga ndani ya mduara wa nne-bora EPL

Na MASHIRIKA

DIEGO Llorente alifungia Leeds United bao la dakika za mwisho na kuwanyima mabingwa watetezi Liverpool fursa ya kutua ndani ya mduara nne-bora kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumatatu usiku.

Liverpool walisajili sare hiyo wakati ambapo suitafahamu inazingira vikosi sita kuu vya EPL ambavyo vimekubali kushiriki kipute kipya cha European Super League (ESL).

Liverpool ya kocha Jurgen Klopp ni miongoni mwa klabu 12 ambazo huenda zikapiga marufuku ya Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) baada ya kutia saini makubaliano ya kunogesha kampeni za ESL.

Kabla ya Liverpool na Leeds United kushuka dimbani, mashabiki wa baadhi ya mashabiki wa Leeds walikusanyika nje ya uwanja wa Elland Road ambapo jezi za Liverpool ziliteketezwa huku ndege ikipaa angani ikiwa na mabango ya kupinga maamuzi ya kuundwa kwa kipute cha ESL.

Ndani ya uwanja, wanasoka wa Leeds United walivalia jezi zenye maandishi “Soka ni ya mashabiki”, ujumbe uliolenga kuashiria kwamba kiini cha kuanzishwa kwa ESL ni msukumo wa wadau kutaka kujinufaisha kifedha.

Liverpool walitamalaki kipindi cha kwanza cha mchezo na wakawekwa kifua mbele na fowadi Sadio Mane aliyeshirikiana vilivyo na beki Trent Alexander-Arnold pamoja na Diogo Jota.

Bao hilo lilikuwa la kwanza kwa Mane kufunga katika EPL tangu Januari 2021 baada ya kushuhudia ukame wa magoli kwenye jumla ya michuano 10.

Chini ya kocha Marcelo Bielsa, Leeds United waliimarika katika kipindi cha pili huku Patrick Bamford akishuhudia kombora lake likigonga mwamba wa goli la Liverpool kabla ya Llorente kumwacha hoi kipa Alisson Becker.

Matokeo ya mechi hiyo yalisaza Liverpool katika nafasi ya sita kwa alama 53, mbili nyuma ya West Ham United wanaofunga orodha ya nne-bora. Leeds United kwa upande wao wanakamata nafasi ya 10 kwa alama 46 sawa na Arsenal.

Iwapo Liverpool watakamilisha kampeni za EPL msimu huu katika nafasi hiyo ya sita, basi huenda wakose hata kufuzu kwa soka ya bara Ulaya muhula ujao iwapo Arsenal wanaofukuzia taji la Europa League au Chelsea wanaowania ubingwa wa Kombe la FA watakosa kuingia ndani ya mduara wa tano-bora kwenye EPL.

Hata hivyo, huenda Liverpool wasihitajike kuhofia chochote iwapo mapendekezo ya kuanzishwa kwa kivumbi cha ESL yataidhinishwa.

Mbali na Jota aliyesajiliwa na Liverpool kutoka Wolves mwanzoni mwa msimu huu, wanasoka wengine waliotatiza ngome ya Leeds United ni Thiago Alcantara na Roberto Firmino waliomwelekezea kipa Illan Meslier makombora mazito.

Ingawa ujio wa Mohamed Salah na Alex Oxlade-Chamberlain uliimarisha kasi ya mchezo kwa upande wa Liverpool, masogora wa Bielsa walisalia imara na wakavuruga kabisa mfumo wa mchezo wa wageni wao.

Leeds United walijizolea alama moja muhimu dhidi ya Liverpool siku saba baada ya kuwakomoa viongozi wa jedwali la EPL, Manchester City kwa mabao 2-1 uwanjani Etihad. Awali, Leeds United walikuwa wamesajili sare ya 1-1 dhidi ya Man-City katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa EPL mnamo Oktoba 3, 2020 ugani Elland Road.

Kibarua kijacho cha Leeds United ni gozi dhidi ya Manchester United ambao wanalenga kujituma maradufu katika mechi zilizosalia ili kuwafikia Man-United kileleni. Chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer, Man-United kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili jedwalini kwa alama 66 na pengo la pointi 10 linatamalaki kati yao na nambari tatu Leicester City.

Liverpool kwa sasa wanajiandaa kualika Newcastle United uwanjani Anfield kwa ajili ya mchuano wao ujao wa EPL mnamo Aprili 24, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Alice Wahome adokeza mgombea mwenza wa Dkt Ruto atatoka...

Johana na timu yake ya Jonkopings waangukia pua ligini...