Michezo

Leeds United wavunja benki na kumng'oa Rodrigo Moreno kutoka Valencia

August 30th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

LEEDS United wamemfanya fowadi mzawa wa Uhispania, Rodrigo Moreno kutoka Valencia sajili wao wa kwanza kadri wanavyojiandaa kunogesha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 16.

Rodrigo, 29, alisajiliwa na Leeds kwa mkataba wa miaka minne baada ya kuweka mezani kima cha Sh3.3 bilioni.

Akiwa Valencia, alifunga jumla ya mabao 59 kutokana na mechi 220 na akasaidia kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kutwaa ubingwa wa Copa del Rey mnamo 2018-19.

Rodrigo anakuwa mchezaji ghali zaidi kuwahi kusajiliwa na Leeds tangu wajinasie huduma za nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, Rio Ferdinand aliyewagharimu Sh2.5 bilioni kutoka West Ham United.

Rodrigo aliwahi pia kuchezea Bolton Wanderers ya Uingereza mnamo 2010-11 kabla ya kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Valencia mnamo 2014 kwa mkopo kutoka Benfica ya Ureno.

Rodrigo, ambaye ni mzawa wa Brazil, alichezea timu ya taifa ya Uhispania kwa mara ya kwanza mnamo 2014 na akaichezea mara 22 huku akifunga mabao manane.

Leeds walipanda ngazi kushiriki kivumbi cha EPL msimu ujao wa 2020-21 kwa mara ya kwanza tangu 2004 baada ya kutawala kilele cha jedwali la Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) msimu huu wa 2019-20.