Leeds United wazamisha chombo cha Southampton

Leeds United wazamisha chombo cha Southampton

Na MASHIRIKA

BAO la mshambuliaji Patrick Bamford lilisaidia waajiri wake Leeds United kusajili ushindi wa 2-0 dhidi ya Southampton katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uliohudhuriwa na mashabiki wa 8,000 uwanjani St Mary’s mnamo Jumanne.

Goli hilo la Bamford lilikuwa lake la 16 katika EPL msimu huu na nusura apachike wavuni mabao mawili zaidi mwishoni mwa kipindi cha pili dhidi ya Southampton ila akazidiwa ujanja na kipa Alex MacCarthy.

Leeds United ya kocha Marcelo Bielsa ilifungiwa goli la pili na kiungo mvamizi Tyler Roberts sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa.

Southampton wanaotiwa makali na kocha Ralph Hasenhuttl walipoteza nafasi nyingi za wazi kupitia fowadi Che Adams aliyeshuhudia mengi ya makombora yake yakipanguliwa na kipa Kiko Casilla.

Ushindi wa Leeds uliwapaisha hadi nafasi ya tisa kwa alama 56 sawa na Everton na moja nyuma ya Arsenal ambao kwa sasa wanafunga orodha ya 10-bora kadri wanavyojiandaa kupepetana na Crystal Palace mnamo Mei 19, 2021 ugani Selhurst Park.

Kwa upande wao, Southampton walisalia katika nafasi ya 14 kwa pointi 44. Ni pengo la alama 15 ndilo linatamalaki kati yao na nambari saba West Ham United watakaopepetana nao katika mchuano wa mwisho wa muhula huu mnamo Mei 23 ugani London Stadium.

Ni mara ya tatu kutokana na misimu 16 iliyopita kwa Southampton kupoteza mechi yao ya mwisho wa msimu katika uwanja wa nyumbani.

Leeds watamenyana na West Bromwich Albion ambao tayari wameshushwa ngazi katika pambano lao la mwisho msimu huu ugani Elland. Jumla ya mashabiki 10,000 wanatazamiwa kuhudhuria gozi hilo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Arsenal kumwachilia Willian ayoyomee Inter Miami...

IEBC yataka waliochochea vurugu Juja wachukuliwe hatua kali...