Leeds United yapepeta Southampton 3-0 katika EPL

Leeds United yapepeta Southampton 3-0 katika EPL

Na MASHIRIKA

PATRICK Bamford alifunga bao lake la 13 katika kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu na kusaidia waajiri wake Leeds United kupepeta Southampton 3-0 mnamo Jumanne usiku.

Bao hilo la Bamford lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na mshambuliaji Tyler Roberts.

Ni ushindi uliowezesha Leeds United ya kocha Marcelo Bielsa kutamatisha rekodi duni ya kupoteza mechi mbili za awali mfululizo. Kwa upande wao, Southampton kwa sasa wamepoteza jumla ya mechi nane mfululizo chini ya mkufunzi Ralph Hassenhutl.

Mabao mengine ya Southampton katika mechi hiyo iliyochezewa ugani Elland Road yalifumwa wavuni kupitia Stuart Dallas na Raphinha.

Wanasoka wengine walioridhisha pakubwa kambini kwa Leeds United ni Jan Vestegaard na Nathan Tella.

Leeds wangalifunga mabao mawili zaidi mwishoni mwa kipindi cha pili ila makombora ya fowadi Diego Llorente yakadhibitiwa vilivyo na kipa wa Southampton.

Fowadi matata wa The Saints, Danny Ings alianza mechi hiyo akiwa benchi na akaletwa uwanjani katika kipindi cha pili japo ujio wake haukutatiza safu ya nyuma ya Leeds waliotamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira.

Leeds kwa sasa wanashikilia nafasi ya 10 jedwalini kwa alama 35 kutokana na michuano 25 iliyopita.

Leeds kwa sasa wana fursa ya kuwaruka Aston Villa jedwalini iwapo watashinda kikosi hicho cha kocha Dean Smith mnamo Februari 27. Kwa upande wao, Southampton wamepangiwa kuchuana na Everton katika mchuano wao ujao mnamo Machi 1 ugani Goodison Park.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mudavadi asisitiza NASA iko kwenye chumba mahututi cha...

Bunge, seneti kuunda kamati moja kuharakisha BBI –...