Michezo

Leicester City kukimbilia Bertrand

June 11th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

LEICESTER City wanatarajiwa kuelekeza macho yao kwa Ryan Bertrand wa Southampton mwenye umri wa miaka 30 iwapo Ben Chilwell atajiunga na Chelsea.

Klabu hiyo inayonolewa na kocha Brendan Rodgers ina matumaini makubwa ya kuvuna Sh5 bilioni iwapo dili ya Chiwell kujiunga na Chelsea itafaulu.

Ni pesa nzuri kumwezesha Rodgers kumtwaa beki huyo wa kushoto ambaye amebakisha mwaka mmoja pekee katika mkataba wake na Southampton.

Kulingana na vyombo vya habari, Bertrand atakubali haraka kujiunga na Leicester City wakati huu klabu hiyo inabakia miongoni mwa nne bora zinazowania nafasi ya kufuzu kwa michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya, msimu ujao.

Hata hivyo, kuna madai kwamba Southampton wanafanya kila wawezalo kuhakikisha beki huyo wa zamani wa Chelsea amebakia klabuni kwa mkataba wa muda mrefu.

Chelsea wanatafuta beki wa kushoto kufuatia madai kwamba kocha Frank Lampard haridhiki na uchezaji wa Marcos Alonso, hasa baada ya madai kwamba naye Emerson anajiandaa kurejea ligi kuu ya Serie A.

Mbali na Chiwell, Chelsea imekamilisha mipango ya kumvutia Timo Werner katika juhudi za kuimarisha kikosi upya.