Leicester City kurefusha mkataba wa fowadi Harvey Barnes ili kusambaratisha mipango ya Liverpool na Man-United

Leicester City kurefusha mkataba wa fowadi Harvey Barnes ili kusambaratisha mipango ya Liverpool na Man-United

Na MASHIRIKA

LEICESTER City wameanzisha mazungumzo na Harvey Barnes kwa nia ya kurefusha mkataba wa sasa wa kiungo huyo mvamizi uwanjani King Power na kuzima matumaini ya Manchester United na Liverpool wanaowania fursa ya kumsajili nyota huyo raia wa Uingereza.

Harvey, 23, anajivunia kuwajibishwa na timu ya taifa ya Uingereza mara moja pekee na amehusika moja kwa moja katika jumla ya mabao 13 ya Leicester huku akifunga magoli tisa katika mechi 24 za hadi kufikia sasa msimu huu.

Ukubwa wa mchango wa Barnes katika ufanisi wa hadi kufikia sasa wa Leicester ni kiini cha Man-United na Liverpool kuanza kumvizia kwa matumaini ya kumtwaa mwishoni mwa msimu huu.

Hata hivyo, kocha Brendan Rodgers anapania kufisha mpango huo wa washindani wao kwa kushawishi Leicester kumpa Barnes mkataba mpya utakaomdumisha ugani King Power kwa kipindi kirefu zaidi.

Kandarasi ya sasa kati ya Barnes na Leicester inatarajiwa kukatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2023-24. Barnes alianza kuchezea akademia ya Leicester akiwa na umri wa miaka 10 pekee.

Alikuwa katika kikosi kilichonyanyulia Leicester ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2015-16.

Kufikia sasa, kikosi hicho kingali miongoni mwa wawaniaji halisi wa taji la msimu huu wa 2020-21 japo pengo la alama 13 linatamalaki kati yao na viongozi wa jedwali, Manchester City wanaojivunia alama 62 baada ya kupepeta West Ham 2-1 mnamo Jumamosi.

Iwapo atatia saini kandarasi mpya, Barnes ambaye kwa sasa hulipwa Sh14 milioni kwa wiki, atakuwa miongoni mwa wanasoka wanaodumishwa kwa ujira mnono zaidi kambini mwa Leicester ambao pia wanahemea huduma za fowadi Jesse Lingard ambaye kwa sasa anachezea West Ham kwa mkopo kutoka Manchester United.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Visa vya uhalifu vyawatia hofu wakazi wa Thika

Brighton wapoteza penalti mbili nalo bao lao la utata dhidi...