Leicester City wacharaza Brighton na kutua nafasi ya pili kwenye jedwali la EPL

Leicester City wacharaza Brighton na kutua nafasi ya pili kwenye jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

DANIEL Amartey alifunga bao mwishoni mwa kipindi cha pili na kusaidia Leicester City kutoka nyuma na kuwapokeza Brighton kichapo cha 2-1 mnamo Machi 6, 2021 uwanjani Amex.

Ushindi huo ulipaisha Leicester ya kocha Brendan Rodgers hadi nafasi ya pili kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 53 na kuweka hai matumaini yao ya kushiriki soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Amartey ambaye ni raia wa Ghana alimwacha hoi kipa wa Brighton, Robert Sanchez aliyeshindwa kufikia mpira wa kona uliochanjwa na kiungo Marc Albrighton katika dakika ya 87.

Kelechi Iheanacho ndiye aliyewarejesha Leicester mchezoni kunako dakika ya 62 baada ya fowadi wa zamani wa Liverpool Adam Lallana kuwaweka Brighton uongozini katika dakika ya 10.

Sasa ni pengo la alama mbili ndilo linawatenganisha Leicester na nambari tatu Manchester United watakaovaana na Manchester City mnamo Machi 7, 2021 ugani Etihad. Man-City ya kocha Pep Guardiola inadhibiti usukani wa EPL kwa alama 65 huku Chelsea wakifunga orodha ya nne-bora kwa pointi 47, moja pekee mbele ya Everton.

Kwa kubwaga Brighton, Leicester waliotawazwa mabingwa wa EPL mnamo 2015-16, waliendeleza rekodi ya kushinda mechi ya 10 mfululizo ligini msimu huu ugenini.

Chini ya kocha Graham Potter, Brighton walisalia katika nafasi ya 16 kwa alama 26 sawa na Leicester. Ni pointi tatu pekee ndizo zinawatenganisha na Fulham ambao kwa pamoja na West Bromwich Albion na Sheffield United, wako katika hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa msimu huu.

Kushuka kwa fomu ya fowadi Jamie Vardy ambaye amefunga bao moja pekee kutokana na mechi 11 zilizopita ligini, kumekuwa kiini cha ufufuo wa Iheanacho – mshambuliaji raia wa Nigeria aliyewahi pia kuchezea Man-City. Iheanacho aliingia ugani kwa ajili ya mechi hiyo akijivunia ufanisi wa kufungia Leicester bao lililowavunia alama moja muhimu dhidi ya Burnley katika mchuano wa awali ligini.

Brighton kwa sasa watakuwa wageni wa Southampton mnamo Machi 14 huku Leicester wakijiandaa kualika Sheffield United siku hiyo ugani King Power.

MATOKEO YA EPL (Machi 6, 2021):

Burnley 1-1 Arsenal

Sheffield Utd 0-2 Southampton

Aston Villa 0-0 Wolves

Brighton 1-2 Leicester

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Raila asihi Wapwani wapitishe BBI

Morata afunga mabao mawili na kusaidia Juventus kuangusha...