Habari Mseto

Leicester City wanyonga Sheffield United na kuweka hai matumaini ya kufuzu kwa Uefa

July 17th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

LEICESTER City waliweka wazi azma ya kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao baada ya kupokeza Sheffield United kichapo cha 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Sheffield United uwanjani King Power mnamo Julai 16, 2020.

Ushindi huo wa Leicester uliwadumisha katika nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 62, moja nyuma ya Chelsea wanaofunga mduara wa tatu-bora.

Leicester walitamalaki kipindi cha kwanza cha mchezo huo huku ushirikiano mkubwa kati ya Jamie Vardy na chipukizi Luke Thomas, 19, ukichangia bao la kwanza lililofumwa wavuni na Ayoze Perez kunako dakika ya 29.

Leicester ya kocha Brendan Rodgers nusura ijipatie bao jingine mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya Harvey Barnes kusalia peke yake na kipa Dean Henderson baada ya kumegewa pasi safi na Vardy.

Mchezaji wa Leicester City Luke Thomas ataka kuurusha mpira wakati wa mechi ya EPL Leicester ikicheza dhidi ya Sheffield United uwanjani King Power Julai 16, 2020. Picha/ AFP

Vardy pia alishuhudia kombora lake nje ya msambamba likibusu mhimili wa lango la Sheffield United ambao kwa wakati fulani katika kipindi cha pili, walionekana kuwazidi nguvu wenyeji wao katika takriban kila idara.

Kiungo mvamizi Demarai Gray ambaye alitokea benchi katika dakika ya 65 kujaza pengo la Barnes ndiye aliyewafungia Leicester bao la pili baada ya kukamilisha pasi nzuri aliyoandaliwa na Vardy kunako dakika ya 79.

Ushindi huo wa Leicester ulikuwa wao wa pili kutokana na jumla ya mechi sita tangu kurejelewa kwa kivumbi cha EPL mnamo Juni 17.

Kwa Sheffield United ambao wanatiwa makali na kocha Chris Wilder, matokeo ya mechi ya jana yalikomesha rekodi nzuri ya kutoshindwa katika jumla ya mechi nne za awali zilizowashuhudia wakiwabwaga Tottenham Hotspur, Wolves na Chelsea.

Sheffield United kwa sasa wanashikilia nafasi ya nane jedwalini kwa alama kwa alama 54, mbili nyuma ya Wolves ambao kwa pamoja na Tottenham, Arsenal na Burnley, wanafukuzia nafasi ya kufuzu kwa soka ya Europa League msimu ujao.

Hata iwapo Sheffield United watakosa fursa ya kufuzu kwa kampeni zijazo za Europa League, Wilder ameshikilia kwamba matokeo ya hadi kufikia sasa yameridhisha mno hasa ikizingatiwa kwamba huu umekuwa msimu wao wa kwanza baada ya kuwa nje ya kipute cha EPL kwa misimu 12 iliyopita.

Leicester kwa sasa wanajiandaa kupimana ubabe na Tottenham ugenini mnamo Julai 19 kabla ya kuwaalika Man-United uwanjani King Power mnamo Julai 26. Kwa upande wao, Sheffield wameratibiwa kupepetana na Everton na Southampton kwa usanjari huo.