Leicester City watoka nyuma na kuendeleza masaibu ya Liverpool katika EPL

Leicester City watoka nyuma na kuendeleza masaibu ya Liverpool katika EPL

Na MASHIRIKA

LEICESTER City walitoka nyuma na kufunga mabao matatu chini ya dakika tano za kipindi cha pili katika ushindi wa 3-1 waliousajili dhidi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Liverpool uwanjani King Power, Jumamosi.

Liverpool waliwekwa uongozini na fowadi Mohamed Salah katika dakika ya 67 baada ya kushirikiana vilivyo na mshambuliaji raia wa Brazil, Roberto Firmino.

Hata hivyo, Leicester ya kocha Brendan Rodgers walirejeshwa mchezoni na kiungo James Maddison aliyemwacha hoi kipa Alisson Becker katika dakika ya 79.

Jamie Vardy ambaye kwa sasa anajivunia magoli 12 kutokana na mechi 24 zilizopita alifungia Leicester bao la pili kunako dakika ya 81 kabla ya Wilfred Ndidi kuchangia bao la tatu lililojazwa kimiani na Harvey Barnes kwa upande wa Leicester katika dakika ya 84.

Liverpool walilazimika kumuondoa uwanjani kiungo James Milner katika dakika ya 17 baada ya kupata jeraha na nafasi yake kutwaliwa na mchezaji wa zamani wa Bayern Munich, Thiago Alcantara.

Leicester ndio walioanza kipindi cha pili kwa matao ya juu na kumleta uwanjani kiungo mvamizi Ayoze Perez kujaza pengo la Marc Albrighton katika dakika ya 74.

Liverpool walijibu mabadiliko hayo ya wenyeji wao dakika moja baadaye kwa kumtoa chipukizi Curtis Jones na nafasi yake kutwaliwa na kiungo wa zamani wa Arsenal, Alex Oxlade-Chamberlain.

Baada ya chombo chao kuzamishwa kwa mabao 3-1, Liverpool walimleta ugani kiungo Xherdan Shaqiri kujaza nafasi ya Georginio Wijnaldum japo hatua hiyo haikuyumbisha Leicester waliosalia imara na badala yake kuwaleta mabeki Hamza Choudhury na Nampalys Mendy kujaza mapengo ya Youri Tielemans na Perez mtawalia.

Ushindi kwa Leicester uliwapaisha hadi nafasi ya pili jedwalini kwa alama 46, moja zaidi kuliko nambari tatu Manchester United ambao watakuwa wageni wa West Bromwich Albion ya kocha Sam Allardyce mnamo Februari 14, 2021 ugani The Hawthorns.

Kwa upande wao, Liverpool wanaotiwa makali na kocha Jurgen Klopp walisalia katika nafasi ya nne kwa pointi 40 na wako katika hatari ya kupitwa na Chelsea, West Ham United na Everton.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Makazi ya kocha Ancelotti yavamiwa mjini Merseyside,...

Solskjaer amfuatilia Erling Braut Haaland kwa nia ya...