Leicester waaibisha Manchester United na kufuzu kwa nusu-fainali za Kombe FA kwa mara ya kwanza tangu 1982

Leicester waaibisha Manchester United na kufuzu kwa nusu-fainali za Kombe FA kwa mara ya kwanza tangu 1982

Na MASHIRIKA

LEICESTER City walitinga nusu-fainali za Kombe la FA kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39 baada ya kuwapokeza Manchester United kichapo cha 3-1 mnamo Jumapili usiku uwanjani King Power.

Leicester walitinga nusu-fainali za Kombe la FA kwa mara ya mwisho mnamo 1982 ila wakabanduliwa na Tottenham Hotspur waliotawazwa wafalme wa taji hilo hatimaye.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer alilaumiwa pakubwa na mashabiki wa Man-United kwa hatua yake ya kupumzisha wanasoka Bruno Fernandes na Luke Shaw kwenye mchuano uliotamalakiwa na Leicester ya kocha Brendan Rodgers kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Fowadi matata raia wa Nigeria, Kelechi Iheanacho alitikisa nyavu za Man-United mara mbili na kujizolea mabao tisa kutokana na mechi tiza zilizopita ndani ya jezi za Leicester.

Sogora huyo aliwaweka Leicester kifua mbele kunako dakika ya 24 baada ya kuchuma nafuu kutokana na masihara ya kiungo Fred na nahodha Harry Maguire na kumwacha hoi kipa Dean Henderson.

Ingawa fowadi chipukizi Mason Greenwood aliwarejesha Man-United mchezoni kwa kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili, kiungo Youri Tielemans aliwaweka waajiri wake Leicester kifua mbele katika dakika ya 52 kabla ya Iheanacho kuzamisha kabisa chombo cha wageni wao katika dakika ya 78.

Licha ya Leicester kukosa huduma za wanasoka mahiri katika mechi hiyo, walijituma ipasavyo na kuwazidi wageni wao maarifa katika takriban kila idara. Kocha Rodgers alikuwa bila viungo wabunifu James Maddison na Harvey Barnes na mabeki James Justin na Wes Morgan wanaouguza majeraha mbalimbali.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Leicester kushinda Man-United baada ya miaka 23.

Iheanacho amekuwa tegemeo kubwa la Leicester msimu huu tangu makali ya Jamie Vardy ambaye kwa sasa amefunga bao moja pekee kutokana na mechi 16 zilizopita kushuka. Iheanacho mwenye umri wa miaka 24, alisajiliwa na Leicester kutoka Manchester City kwa kima cha Sh3.5 bilioni mnamo Agosti 2017.

Leicester kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Manchester City na West Ham United katika michuano yao ijayo ligini na watakutana na Southampton kwenye nusu-fainali za Kombe la FA. Leicester wanapigiwa upatu wa kumaliza kampeni za EPL msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora na kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao. Kikosi hicho kiliwacharaza Southampton 9-0 katika mechi ya EPL uwanjani St Mary’s mnamo 2019-20.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Haaland aokotea Dortmund pointi moja dhidi ya Cologne...

Onyo magaidi wasajili watoto mitandaoni