Michezo

Leicester wapepeta Leeds United na kutua nafasi ya pili kwenye jedwali la EPL nyuma ya Liverpoool

November 3rd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

NYOTA Youri Tielemans alifunga mabao mawili na kusaidia Leicester City kusajili ushindi wa 4-1 dhidi ya limbukeni Leeds United katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowakutanisha uwanjani Elland Road mnamo Novemba 2, 2020.

Ushindi huo wa Leicester uliwakweza hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 15, moja pekee nyuma ya viongozi na mabingwa watetezi, Liverpool.

Mshambuliaji Jamie Vardy alihusika katika mabao mawili ya kwanza ya Leicester baada ya kushirikiana na Harvey Barnes katika kipindi cha kwanza na kusaidia Leicester kuchuma nafuu kutokana na masihara ya beki Robin Koch.

Tielemans alipachika wavuni bao la pili la waajiri wake kunako dakika ya 21 kabla ya Stuart Dallas kurejesha Leeds United mchezoni mwanzoni mwa kipindi cha pili. Bao lililofungwa na Leeds liliamsha hasira ya Leicester waliofungiwa na Vardy katika dakika ya 76 kabla ya Tielemans kuzamisha chombo cha wenyeji wao kupitia penalti ya mwisho wa kipindi cha pili.

Chini ya kocha Marcelo Bielsa, Leeds walionekana kuzidiwa maarifa katika takriban kila idara huku idara yao ya uvamizi ikisalia butu kutokana na kutokuwepo kwa sajili mpya Rodrigo Moreno aliyelazimika kujitenga baada ya kutangamana na mtu aliyepatikana na virusi vya corona mwanzoni mwa wiki.

Mbali na Patrick Bamford aliyenyimwa nafasi ya wazi na kipa Kasper Schmeichel, wanasoka wengine wa Leeds waliopoteza nafasi nyingi za wazi ni Barnes na Pablo Hernandez.

 

Kiungo wa Leicester City, Mbelgiji Youri Tielemans asherehekea baada ya kuifungia bao la nne ikicheza dhidi ya wenyeji Leeds United katika uwanja wa Elland Road, Novemba 2, 2020, ambapo wageni walipata ushindi wa 4-1. Picha/ AFP

Ushindi uliovunwa na Leicester ulikuwa wao wan ne mfululizo, ufanisi unaorejesha ufanisi wa msimu uliopita ambao walianza kampeni hizo kwa matao ya juu kabla ya kutepetea katika majuma ya mwisho. Ni ufanisi ambao pia uliwasaidia kufikia rekodi ya 2000-01 ambapo walitia kapuni jumla ya alama 15 kutokana na mechi saba za mwanzo wa msimu.

Leicester wamesajili ushindi katika kila mojawapo ya mechi kati ya nne zilizopita msimu huu. Hiyo ni mara yao ya kwanza tangu waanze kupiga soka ya EPL miaka 116 iliyopita.

Leeds kwa sasa wamepoteza mechi mbili mfululizo ligini kwa mara ya kwanza chini ya kocha Bielsa. Mara yao ya mwisho kushuhudia hayo ni mnamo Machi 2018 chini ya mkufunzi Paul Heckingbottom.

Stuart Dallas anakuwa mchezaji wa kwanza raia wa Northern Ireland baada ya Nigel Worthington mnamo Disemba 1994 dhidi ya West Ham United kuwahi kufungia Leeds United ligini.

Leeds United waliorejea kushiriki EPL msimu huu baada ya miaka 16, kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Crystal Palace uwanjani Selhurst Park mnamo Novemba 7 huku Leicester wakiwaalika Sporting Braga kwa gozi la Europa League mnamo Novemba 5, kabla ya kushuka dimbani kuvaana na Wolves katika EPL mnamo Novemba 8, 2020.