Michezo

Leicester wasajili Fofana kutoka St-Etienne kwa miaka mitano

October 3rd, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

LEICESTER City wamemsajili beki Wesley Fofana kutoka Saint-Etienne kwa mkataba wa miaka mitano.

Kiungo huyo chipukizi mwenye umri wa miaka 19, ameingia katika sajili rasmi ya Leicester almaarufu ‘The Foxes’ kwa kiasi kisichojulikana cha fedha.

Fofana alivalia jezi za kikosi cha kwanza cha St-Etienne katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Mei 2019 na akawa sehemu ya kikosi kilichopigwa na Paris Saint-Germain (PSG) kwenye fainali ya French Cup mnamo Julai 2020.

“Nina furaha kuwa hapa. Nimekuwa nikifuatilia Leicester City kwa karibu sana tangu watawazwe mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2015-16,” akasema Fofana.

Beki huyo alijumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa cha U-21 na anapigiwa upatu wa kuunga kikosi cha kwanza cha Leicester dhidi ya West Ham United mnamo Oktoba 4, 2020.

Fofana anakuwa sajili wa tatu wa Leicester kufikia sasa muhula huu baada ya kikosi hicho kujitwalia huduma za beki Timothy Castagne kutoka Atalanta na fowadi Cengiz Under aliyetokea AS Roma nchini Italia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO