Habari Mseto

LEILA WANGARI: Niko tayari kukosolewa na manguli wa uigizaji

April 21st, 2019 2 min read

Na JOHN MIMWERE

AMEBISHA! Ameanza kupiga ngoma huku akilenga kukwea milima na mabonde ili kufikia levo ya kimataifa katika tasnia ya uigizaji. Amehitimu kutoka Chuo Kikuu cha Moi kwa shahada ya digrii katika masuala ya hoteli za kifahari.

Anasema ingawa ndiyo ameanza uigizaji ni taaluma iliyokuwa ndoto yake tangu akiwa mdogo ambapo amepania kujituma kisabuni akilenga kuibuka kati ya waigizaji mahiri duniani miaka ijayo.

Anasema alianza kujituma kwenye masuala ya uigizaji akiwa mwanafunzi kwenye shule ya upili ya Karoti Girls High.

Leila Wangari (28) anajivunia kushiriki filamu ya kwanza iliyozinduliwa mapema mwezi huu iitwayo ‘The Lady in Red‘ iliyotengenezwa na kundi la Son of Man International.

”Hakika nilifurahi sana filamu hiyo ilipokelewa vyema na Wakenya waliofurika tele katika ukumbi wa Kenya National Theatre siku ya uzinduzi,” alisema na kuongeza kwamba hawana budi ila kuwashukuru wote waliojitokeza kuunga mkono filamu ya wazalendo.

Dada huyu anasema analenga kujikaze awezavyo katika uigizaji angalau afikie viwango vya Wakenya wanaofanya kweli duniani akiwamo Eddy Gathegi na Lupita Nyongo anayetamba katika filamu za Hollywood.

Binti huyu anasema amejifunga kimbwembwe kusoma vitabu mbalimbali kuhusu masuala ya uigizaji ili kujiongezea maarifa. ”Vile vile niko tayari kukosolewa na waliotangulia mradi wanapania kunijenga katika masuala ya uigizaji,” aliambia Taifa Leo Dijitali.

Mwigizaji Leila Wangari. Picha/ John Kimwere

Katika mpango mzima anapenda kutazama vipindi mbali mbali ili kujifunza zaidi masuala ya uigizaji ikiwamo Tahidi High (Citizen TV), House of Kawangware (KTN TV), Selina na Vashita (Maisha magic East DStv).

Aidha anashukuru binamu yake Marvin Kibicho anayesema kwamba amepiga hatua katika uigizaji maana amekuwa mstari wa kwanza kwa kumtia motisha. Anaamini ndiyo mwanzo wa ngoma na siku sijazo atashiriki filamu zitakazopata mpenyo kuonyeshwa kwenye baadhi ya runinga za hapa nchini.

Chipukizi huyu anadokeza kuwa pia anapenda kutazama kazi zake staa wa Marekani Jenipher Aniston ambaye ameigiza filamu kama ‘Horrible Bosses,’ ‘Dumplin,’ ‘Were The Millers,’ na ‘Just Go With It,‘ kati ya zingine. Staa huyo anasema kuwa amekomaa katika taaluma hiyo maana anaweza kuigiza nafasi yoyote.

Anahimiza mwenzake wanaokuja kutovunjika moyo licha ya kushiriki majaribio mara nyingi bila kufaulu maana ipo siku milango itafunguka.

Kadhalika anawashauri kuwa wafahamu malengo yao katika sekta ya filamu wala wasikubali kushushwa hadhi na maprodyuza mafisi.

Anawataka waigizaji wa kike kujitolea vilivyo wanapopata nafasi ya kuigizaji filamu yoyote ili kutambuliwa kwa kazi zao.

Kadhalika anazitaka serikali za kaunti bila kuweka katika kaburi la sahau serikali ya kitaifa kuwekeza katika sanaa ya uigizaji ili kutoa nafasi za ajira kwa wasanii wanaoibukia.