NA RICHARD MUNGUTI
ADHABU ya kifo iliyopitishwa dhidi ya afisa wa polisi aliyewaua kinyama wakili Willie Kimani, mteja Josephat Mwenda na dereva wa teksi Joseph Muiruri mwaka 2016 imepokelewa kwa furaha na shangwe na familia za wahanga hao waliopoteza maisha bila hatia.
Wameambia Taifa Leo “haki imefanyika baada ya kuisubiri kwa miaka saba.”
Sajini Fredrick Leliman amehukumiwa anyongwe kwa kutiwa kitanzi. Jaji Jessie Lesiit ndiye ametoa hukumu hiyo.
Jaji Lesiit alisikiliza kesi hiyo kwa miaka sita na kupokea ushahidi kutoka kwa watu 46.
Amesema polisi walioongozwa na Bw Nicholas ole Sina walitumia teknolojia na taarifa za mawasiliano ya washtakiwa ya simu kuthibitisha kesi hiyo.
Mbali na Leliman, Jaji Lesiit amewahukumu maafisa wa polisi Stephen Cheburet na Sylvia Wanjiku miaka 30 na 24 mtawalia. Wawili hawa ndio waliowafungia Kimani, Mwenda na Muiruri ndani ya kontena katika kituo cha polisi wa utawala cha Syokimau kabla ya kutolewa usiku wa Juni 23/24,2016 na kuuawa kinyama.
Mdokezi wa maafisa hao Peter Ngugi aliyefichua jinsi Kimani, Mwenda na Muiruri walitekwa nyara kutoka mahakama ya Mavoko, kuuawa na miili yao kutupwa mtoni Athi River eneo la Donyo Sabuk, amesukumwa jela miaka 20.
Wajane Annah (mjane wa Willie Kimani) na Rebecca (mjane wa Josephat Mwenda) pamoja na watu wa familia zao na mashirika ya kutetea haki za binadamu na Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) wamepongeza Jaji Lesiit kwa kutekeleza haki licha ya kuisubiri kwa miaka saba.
Akitoa adhabu, Jaji Lesiit amesema “Leliman alipanga njama ya jinsi ya kumuua Josephat Mwenda aliyekuwa na uadui na kisasi naye bila sababu kwa muda mrefu.”
Leliman alikuwa amemfungulia mashtaka Mwenda na hata wakati mmoja alimpiga risasi ya mguu.
Ni kutokana na uhasama huo ambapo Mwenda alitafuta usaidizi kutoka kwa shirika la kimataifa la International Justice Mission (IJM) lenye makao yake makuu nchini Amerika.
IJM ilimwagiza Kimani amtetee Mwenda.
IJM na mamlaka huru ya polisi IPOA ilianza kumchunguza Leliman ndipo akaapa kumwangamiza Mwenda akiteta “ameniharibia kazi.”
Jaji Lesiit alisema Leliman aliweka mikakati ya kumwangamiza Mwenda kwa kumfungulia kesi mbili katika mahakama ya Mavoko, Athi River kaunti ya Machakos.
Leliman aliyeelezwa na Jaji Lesiit kuwa hatari kwa usalama kwa umma pia alikuwa amemsingizia Mwenda anauza mihadarati na alikuwa akibeba abiria wengi kwa pikipiki yake.
Mnamo Juni 23, 2016, Mwenda alitakiwa kufika katika mahakama ya Mavoko kuendelea na kesi hizo.
Ni wakati huo Leliman alimtuma mdokezi Peter Ngugi almaarufu Brown mahakamani kufuatilia mienendo ya wakili Kimani na Mwenda.
Kimani alikuwa amekodisha teksi ya Joseph Muiruri kumpeleka mahakamani Mavoko pamoja na Mwenda.
Jaji Lesiit alisema Ngugi alimwarifu Leliman kwamba watatu wametoka kortini na wameabiri teksi ya Muiruri.
Leliman aliwasubiri katika kivuko cha Reli Athi River na kuwateka nyara Kimani, Mwenda na Muiruri.
Aliwaigiza kwa gari lake na kumwagiza mtu mwingine ambaye hajawahi kukamatwa hadi sasa aipeleke teksi ya Muiruri eneo la Kamirithu, Limuru na kuliacha hapo.
Jaji Lesiit alisema Leliman aliwapeleka watatu hao katika korokoro ya kituo cha polisi cha Syokimau na kuwafungia ndani ya kontena.
Watatu hao walitolewa usiku wa Juni 23, 2016 na kupelekwa kwenye shamba lililo karibu na Nation Printing Press na kuwaua kinyama.
Leliman na maafisa wa polisi wenzake walitia miili ya Kimani, Mwenda na Muiruri ndani ya magunia.
Pia walifunga vichwa vyao kwa mifuko ya dukakuu la Mullei na kuisafirisha miili hadi mto Athi River eneo la Ol Donyo Sabuk na kuitupa hapo Juni 24, 2016.
Maiti hizo zilipatikana Juni 30, 2016 kama zimeoza.
Jaji Lesiit alisema vitendo vya wanne hao ni vya kinyama na kamwe hawana utu.
Wafungwa hao walipewa siku 14 kukata rufaa.
Wakili Cliff Ombeta aliyewakilisha Leliman na Cheburet amesema haki haikutendeka na kwamba Jaji Lesiit hakuzingatia ushahidi aliowasilisha na kwamba atakata rufaa.
“Leliman na Cheburet hawakuwa mahala Kimani na wenzake waliuawa,” Ombeta amesema baada ya uamuzi kutolewa.
Ngugi ameomba arudishwe katika gereza la Naivasha kwa sababu za usalama wake.
Ngugi ndiye alifichua jinsi Kimani na wenzake walivyouawa.