Lempurkel aomba aachiliwe kwa dhamana kabla ya kesi kuamuliwa

Lempurkel aomba aachiliwe kwa dhamana kabla ya kesi kuamuliwa

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA mbunge wa Laikipia kaskazini Mathew Lempurkel anayetumikia kifungo cha mwaka mmoja kwa kumtandika mbunge wa sasa Sarah Korere miaka mitano iliyopita amewasilisha rufaa katika Mahakama kuu.

Bw Lempurkel alimchapa kofi na kumtandika teke tumboni Bi Korere wakati wa farakano katika afisi ya aliyekuwa waziri wa usalama Joseph Nkaissary Novemba 2016. Mfungwa huyo anaomba mahakama kuu imwachilie kwa dhamana kutoka gerezani kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa rufaa aliyowasilisha kupitia kwa wakili wake Saitabao ole Kanchori.

Katika rufaa hiyo , Lempurkel amesema hakimu mwandamizi Hellen Onkwani aliyesikiza kesi hiyo hakuzingatia sheria ipasavyo alipomuhukumu. Lempurkel amesema , Sarah ndiye alimchokoza na kumsambulia mbele ya marehemu Nkaissery huku madiwani 20 wakitazama kwa mshangao.

“Hakimu aliyesikiza kesi hii hakuzingatia sheria alipokataa kuangazia ushahidi wa walioshuhudia farakano kati ya Sarah na Lempurkel huku wafuasi wa mbunge huyo wakishuhudia,” Bw Kanchori asema katika rufaa aliyowasilisha. Mbunge huyo wa zamani alifungwa Novemba 5,2021 baada ya kupatikana na hatia ya kumpiga na kumwumiza Sarah.

Wakili huyo anadai Bi Onkwani alipuuza ushahidi kuwa Lempurkel na Sarah ni mahasidi sugu kisiasa. Katika rufaa hiyo alieleza uamuzi huo wa Bi Onkwani wa kiimla na usiozingatia vipengee vya kutoa adhabu kali ikitiliwa maanani mlalamishi alikwaruzwa tu.

Bw Kanchori ameongeza kusema kuwa kwa vile mfungwa huyo anatazamia kuwania kiti cha ubunge wa eneo hilo la Laikipia kaskazini kifungo cha mwaka mmoja kinalenga kumzuia asishiriki katika zoezi hilo la Agosti 9 2022. “Kifungo hiki kinaonekana kwamba kinasukumwa kisiasa hali inayoshusha imani ya umma katika idara ya mahakama,” asema wakili huyo.

Bw Kanchori anaomba mahakama imwachilie kwa dhamana Lempurkel kwa vile rufaa aliyowasilisha itakubaliwa na kifungo kufutiliwa mbali.Jaji Lilian Mutende ameorodhesha kusikiza rufaa hiyo mnamo Desemba 6,2021.

You can share this post!

Washukiwa wanne wakamatwa kwa kudaiwa kuiba nyaya za stima...

Olunga aibuka Mfungaji Bora dimba la Asia kwa mabao 9

T L