Habari Mseto

Lenaola kuitwa kwa kesi ya umiliki wa mali ya Sh700m

June 5th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WAFANYABIASHARA wawili watamwita Jaji wa Mahakama ya Juu Isaac Lenaola kutoa ushahidi katika kesi ya umiliki wa mali ya Sh700 milioni.

Mabw Kuldip Sapra na Ashman Sapra walimweleza hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku kuwa wangelipenda Jaji Lenaola afike kortini kueleza iwapo waliapishwa mbele yake kumlaghai mali mke wa ndugu yao Dkt Nisha Sapra.

Mabw Sapra wanaopinga kushtakiwa tena katika mzozo wa umiliki wa mali aliyoacha ndugu yao Yogash Mohan Madan Sapra walimweleza Bi Mutuku kuwa hawakughushi stakabadhi yoyote ya mahakama kumlaghai Dkt Sapra anayeshtakiwa kwa mauaji ya mumewe Septemba 5, 2008.

Wawili hao wamewasilisha ombi la kupinga wakifunguliwa mashtaka ya kufanya njama za kumlaghai Dkt Sapra.

Mawakili Harun Ndubi na Miller Bwire walimweleza hatua ya Mkurugenzi wa Mashtaka yaUmma DPP Noordin Haji ya kuwashtaki kwa ulaghai ni matumizi mabaya ya mamlaka aliyopewa kisheria.

Bw Ndubi alisema hakuna maagizo yoyote waliyopewa ndugu hao na mahakama kumpokonya mjane huyo.

Wakili huyo alisema kuwa hati wanazodaiwa waliiba ni fomu zinazotolewa na mahakama na kutiwa saini na mawakili na wala sio wanaowasilisha maombi.

Pia walimweleza hakimu huyo kwamba Dkt Sapra anayeshtakiwa kwa mauaji ya mumewe hawezi tambuliwa kama mlalamishi ikitiliwa maanani anakabiliwa na shtaka la kumuua mumewe.

Wawili hao wamesema Dkt Sapra ametajwa kuwa mmoja wa wale watakaofaidi na mali ya marehemu mumewe.