Michezo

Lengo la Kahawa Queens ni kutesa mabinti wapinzani ligini

May 26th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wanawake ya Kahawa United ambayo sasa itajulikana kama Kahawa Queens inalenga kupigana kwa udi na uvumba kwenye mechi za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza msimu huu.

Ujio wa kikosi kushiriki ligi ya kiwango hicho unatarajiwa kubadilisha kampeni za ngarambe ya mwaka huu.

Kuna uwekanao mkubwa huenda Kahawa Queens ikachochea washiriki wengine na kuzinduka kwenye mechi za kuwinda ubingwa wa taji hilo msimu huu.

”Tayari tumeanza maandalizi ya kushiriki michuano ya msimu huu ingawa timu zingine zimepiga raundi tatu,” kocha wa kikosi hicho, Joseph Wambua alisema na kuongeza kwamba anaaminia wachezaji wake wameiva vya kutosha hata kushiriki mechi za Soka la Ligi Kuu nchini (KWPL) hamna tatizo.

Wachezaji wa timu hii wamefanya mazoezi tosha hasa jinsi ya kugaragaza gozi ya ngombe.

Kikosi hicho kinajumuisha baadhi ya wasichana wepesi kama nahodha wake pia mchezaji wa Harambee Starlets, Neddy Atieno.

Wanawake wa kikosi hicho hupiga gozi ya ngombe kukaribia kiwango cha wanaume.

”Kusema ukweli wachezaji wangu pia wanataka zaidi kushiriki michezo ya Ligi za hadhi ya juu nchini,” kocha huyo alisema.

Kahawa United ilibeba tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki kipute hicho ilipobamiza JYSA FC kwa mabao 5-0 katika fainali iliyopigiwa Uwanjani Kenyatta Stadium, mjini Machakos. Kipindi cha kwanza Kahawa United ilishuka dimbani bila huduma za wachezaji wawili muhimu Neddy Atieno na Everline Juma na kutoka nguvu sawa sare tasa.

Baada ya pande zote kukosa kufungana kipindi cha kwanza, kipindi cha lala salama, JAYSA FC ilijikuta njia panda kufuatia ujio wa wawili hao. Nahodha huyo alicheka na wavu mara tatu nao Magaret Atieno na Patricia Amase kila mmoja akiitingia bao moja.

“Tayari tumeanza kupiga shughuli zetu safi maana tumepania kufuzu pia kupandishwa ngazi kushiriki mechi za Ligi Kuu nchini (KWPL) hivi karibuni,” nahodha wa Kahawa United alisema.

Awali kwenye mechi za kusaka tiketi ya kusonga mbele, Kahawa United iliinyamazisha Kangemi Ladies kwa mabao 3-0 katika fainali ya kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) iliyosakatiwa Camp Toyoyo Jericho, Nairobi.

Kahawa United imejiunga na vikosi vingine ikiwemo Sunderland Samba FC, Limuru Starlets, Soccer Sisters na Joylove FC. Pia zipo Mukuru Talent Academy, Moving The Goalposts (MTG) na Mombasa Olympic.

Kahawa United ilimaliza mechi za Nairobi East Regional League (NERL) kileleni kwa kuzoa alama 32 bila kupoteza mechi yoyote baada ya kushinda mechi kumi na kutoka nguvu sawa mara mbili.

Kadhalika kocha huyo alisema ”Nina imani na timu yangu huenda tukashiriki mechi divisheni wani msimu huu pekee kisha tufanye kweli na tupande ngazi maana vipusa wangu wamejaa motisha ya kweli michezoni.’