Lengo la Uingereza kwa sasa ni kutwaa Kombe la Dunia 2022 – kocha Gareth Southgate

Lengo la Uingereza kwa sasa ni kutwaa Kombe la Dunia 2022 – kocha Gareth Southgate

Na MASHIRIKA

KOCHA Gareth Southgate amesema kwamba kubwa zaidi katika malengo yake kwa sasa ni kuongoza Uingereza kunyanyua Kombe la Dunia mnamo 2022 kabla ya kuachilia mikoba ya kikosi hicho.

Hii ni baada ya mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 50 kushindwa kusaidia kikosi chake kutwaa taji la Euro mwaka huu katika fainali ya kwanza ya soka ya haiba kubwa kwa Uingereza kushiriki tangu wanyakue Kombe la Dunia mnamo 1966.

Uingereza almaarufu Three Lions walipokezwa kichapo cha 3-2 kupitia penalti kutoka kwa Italia baada ya kuambulia sare ya 1-1.

Southgate pia amefichua kwamba asingependa kurefusha zaidi kipindi cha kuhudumu kwake kambini mwa Uingereza iwapo kikosi hicho kitashindwa kutia kapuni Kombe la Dunia kwenye fainali zijazo.

Mkataba wa sasa kati ya Uingereza na kocha huyo anayelipwa Sh546 milioni kwa mwaka, unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa 2022.

“Nisingetaka kusalia kuwa kocha wa Uingereza kwa kipindi kirefu zaidi iwapo hatutatwaa Kombe la Dunia nchini Qatar,” akasema kocha huyo ambaye hakuwahi kuchezesha kikosi kimoja zaidi ya mara mbili kwenye fainali za Euro mwaka huu huku akikumbatia mifumo ya 4-3-3, 3-4-3, 5-2-3 na 4-2-3-1 katika michuano mbalimbali ya kipute hicho.

Uingereza hawakufungwa bao lolote kwenye kampeni hizo za Euro hadi hatua ya nusu-fainali ambapo Mikkel Damsgaard alimzidi maarifa kipa Jordan Pickford. Uingereza walishinda mechi hiyo 2-1 na kufuzu kwa fainali. Bao lao dhidi ya Italia kwenye fainali lilifungwa na beki Luke Shaw kabla ya Leonardo Bonucci kusawazisha.

“Sasa macho na mawazo yetu yanaelekezwa kwa fainali za Kombe la Dunia. Tutakuwa na kila sababu ya kutwaa taji hilo kwa kuwa kikosi hiki kina idadi nzuri ya chipukizi wanaozidi kuimarika kila uchao,” akaongeza Southgate.

Kocha huyo ambaye ni mchezaji wa zamani wa Uingereza, aliongoza Three Lions kutinga fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi. Hata hivyo, walidenguliwa na Croatia kwa kichapo cha 2-1.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Barcelona wamtia Messi kwenye orodha ya masogora...

SHINA LA UHAI: HIV: Maelfu wakwepa tembe za PrEP,...