Lengo ni kusalia kwa tano bora ligini – Mwatate FC

Lengo ni kusalia kwa tano bora ligini – Mwatate FC

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

NI wanagenzi katika ushiriki wao wa Supaligi ya Taifa, lakini wamekataa kuonyesha udhaifu ama kuwa kutokana na ugeni wao katika ligi hiyo, waonyeshe unyonge.

Mwatate United FC imekuwa ikipigania kupanda ngazi kutoka Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza miaka kadhaa iliyopita, ikitoa ahadi kuwa itakapopanda hadi Supaligi, itajitahidi kuhakikisha kuwa inafanya vizuri.

Wakati imeshacheza mechi 12 za mwanzo katika ligi hiyo ambayo washindi wake wawili wanapanda hadi Ligi Kuu ya FKF, Mwatate United imedhihirisha kuwa kilio chao cha kutaka kupanda ngazi kilikuwa cha haki na wamepania kufanya maajabu katika ligi hiyo.

Timu nyingine mbili za jimbo la Pwani zilizoko katika ligi hiyo, moja ya Coast Stima FC ndiyo iko juu kwenye ngazi ya ligi hiyo ikiwa kwenye nafasi ya tano lakini Mwatate imeipiku hiyo nyingine ya Modern Coast Rangers FC.

Katika ngazi ya ligi hiyo, Mwatate iko katika nafasi ya sita ikiwa na pointi 19 hali Modern Coast iko nafasi ya 12 ikiwa na pointi 15.

Timu ya Coast Stima inasafiri hadi Kisumu kupambana na Kisumu Hot Stars kwenye mechi ambayo vijana hao wa pwani wanataka kwa vyovyote vile washinede ili wasifikiwe ama kupitwa na Mwatate ama Modern Coast. Timu ya Kenya Police iko kileleni ikiwa na jumola ya pointi 22.

Mwenyekiti wa Mwatate United FC, James Okoyo anasema wamepania mara hii kujitahidi kumaliza japo nafasi ya tatu hadi tano bora kwa sababu wangali ni wageni kwenye ligi hiyo. “Tunachotaka ni kufanya vizuri ili tuweze kujiandaa kupigania ushindi msimu ujao wa 2021-2022,” akasema Okoyo.

Kikosi cha msimu huu cha Mwatate United FC kina Godfrey Wakabu, Farouk Mudola, Geioffrey Onjuati, Dennis Ochieng, Cornellius Mwangi, Nigol Mohamed, Cornellius Juma na Joseph Nsobya.

Wengine ni Stephen Mweni, Robinson Joshua, John Musyoka, Salim mwakulomba, John Msau, Granton masha, Gideon Mwamburi, Dennis Ouma, Evans Mumu, Dishan Mareko, Oscar Oketch, Morvin Otinya, Paul Otini, Victor Otieno na Francis Mwangi.

Maafisa wa benchi la ufundi ambao wanaishikilia na kuiendeleza timu hiyo ni Kocha Mkuu Rix Kanuli, Meneja Christopher Nyamao na Naibu Kocha Mark Otieno.

Kanuli amewapongeza wachezaji wake kwa jinsi wanavyopigana wanapocheza mechi zao za nyumbani na ugenini na akaeleza matumaini makubwa ya timu hiyo kufanya vizuri na kumaliza ligi kwenye nafasi nzuri.

“Tuko nafasi bora hivi sasa ya nane ambayo si mbaya kabisa lakini nina matumaini hivi tunavyoendelea kupata uzoefu, tutazidi kufanya vizuri na tutapanda. Nia yetu kubwa ni tusishuke chini ya nafasi ya tano,” akasema Kanuli.

Kufikia kiwango hichi cha sasa, mashabiki wa jimbo la Pwani wanaamini Mwatate ikipata kusaidiwa zaidi kwa wachezaji wawili ama watatu na kwa fedha za kuendesha timu hiyo, inaweza haraka hata msimu huu, kushinda na kupanda hadi ligi kuu.

Kanuli anasema ushindi uliompendeza zaidi ni uole wa Pwani Dabi kati yao na Modern Coast Rangers FC kwani pambano hilo lilikuwa la kupendeza na ambalo kila timu iling’ang’ania ushindi ipate kupanda ngazi hna kuwa nafasi nzuri.

“Ninawapongeza wachezaji wangu wote ambao waliingia uwanjani wakiwa wana nia ya kuhakikisha wanaondoka Mombasa wakiweka kibindoni pointi zote tatu. Nia hiyo waliitekeleza kwa vitendo na tunajiandaa kwa mechi yetu ijayo dhidi ya Kibera Black Stars,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Morans yaimarika kwenye viwango bora vya mpira wa vikapu...

Sofapaka kuwa na kikosi kamili dhidi ya Bidco United