Michezo

Leno aamini Spurs na Arsenal watatinga Nne-bora

April 24th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MNYAKAJI wa Arsenal Bernado Leno ametabiri kwamba Arsenal na Tottenham ndizo timu zitakazoungana na Manchster City na Liverpool ili kukamilisha orodha ya timu nne zitazofuzu kushiriki Klabu Bingwa Barani Ulaya(UEFA) msimu ujao wa 2019/20.

Arsenal maarufu kama The Gunners wanashikilia nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza(EPL), alama moja nyuma ya Chelsea ingawa bado hawajawajibikia mechi moja.

Nambari tatu Tottenham Hot Spurs wana alama 70 baada ya kufunga bao dakika za jioni kwenye mechi dhidi ya Brighton Jumanne usiku.

Akizungumza kabla ya mechi kati ya Spurs na Brighton, mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya Ujerumani alisema anatarajiwa klabu yake na Spurs ambazo zina makao katika mji wa London kutwaa nafasi mbili zilizosalia.

“Manchester City wanashinda EPL, Liverpool wamalize katika nafasi ya pili kwa kuwa wana mchuano wa UEFA ambao utawamaliza nguvu. Hata hivyo naamini wanaweza kubwaga Barcelona kwenye nusu fainali huku Man City wakibeba pia Kombe la Shirikisho la Soka nchini Uingereza(FA),” akasema Leno.

“Naamini Arsenal itafuzu na sasa hatima hiyo ipo mikononi mwetu. Siyazingatii matokeo ya timu nyingine kwasababu tunahitaji tu kushinda mechi zilizosalia ili tuwe pazuri,” akaongeza.