LEONARD ONYANGO: CBC isiwabague watotowatokao familia maskini

LEONARD ONYANGO: CBC isiwabague watotowatokao familia maskini

Na LEONARD ONYANGO

IDARA mpya iliyobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Wizara ya Elimu ili kusimamia utekelezaji wa mfumo mpya wa Elimu ya Umilisi (CBC) inafaa kuweka usawa kuhakikisha kuwa watoto kutoka familia maskini hawaachwi nyuma.

Rais Kenyatta, wiki iliyopita, aliunda idara mpya na kuitwika jukumu la kuhakikisha kuwa mfumo wa elimu ya 2-6-6-3 unatekelezwa kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na jopokazi la wataalamu 26 walioongozwa na msaidizi wa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kenyatta Fatuma Chege.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na jopokazi hilo ni kwamba serikali iweke mikakati ya kuelimisha wazazi kuhusu majukumu yao katika mfumo huo wa CBC.

Pendekezo hilo, huenda lilitokana na ukweli kwamba baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwafanyia watoto wao kazi wanazopewa na walimu kufanyia nyumbani badala ya kuwapa mwongozo.

Tangu mfumo wa CBC kuanza kutekelezwa humu nchini miaka minne iliyopita, kumekuwa na malalamishi kuhusu gharama ya juu ambapo wazazi wanalazimika kutumia kiasi kikubwa cha fedha kununulia vifaa vinavyohitajika shuleni.

Mfumo wa CBC umebandikwa jina la ‘mtaala wa matajiri’ kutokana na vifaa vingi vinavyohitajika shuleni ambavyo maskini hawawezi kumudu.Kwa mfano, baadhi ya wazazi wamekuwa wakitakiwa kununua faili, vitabu, karatasi ngumu, Biblia, Kamusi na vifaa vinginevyo vingi vinavyohitajika katika masomo ya CBC.

Wazazi wanapewa kazi ya kupiga picha watoto wao wakifanya shughuli mbalimbali nyumbani. Wazazi wanatakiwa kupakua picha au video mitandaoni na kupeleka shuleni.

Baadhi ya shule pia zinawataka wazazi kununua vifaa vya kilimo kama vile wilibaro, vyombo vya jikoni, nakadhalika.Ukweli ni kwamba idadi kubwa ya Wakenya maskini hawana simu za kupiga picha watoto wala intaneti ya kupakulia video au picha mitandaoni. Changamoto hiyo huenda ikasababisha watoto kutoka familia maskini wakasalia nyuma katika masomo yao.

Taasisi ya Ukuzaji wa Mtaala (KICD) mwaka jana ilijitetea kuwa walimu wamekuwa wakiwaongezea wazazi mzigo wa kununua vifaa vya masomo kwa sababu hawajaelewa vyema CBC.Bi Olive Mbuthia, Naibu Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi wa KICD, alilaumu walimu ambao hawajaelewa mfumo wa CBC kwa kuwatwika wazazi mzigo mzito wa kununua vifaa kama vile wilibaro, vyombo vya jikoni kati ya vinginevyo.

Ikiwa walimu waliopewa mafunzo kabla ya kuanza kufundisha CBC ndio hawajaelewa vyema; hiyo ni ishara kwamba idadi kubwa ya Wakenya hawaelewi kinachoendelea.

Serikali haina budi kuhakikisha kuwa inatoa mafunzo kwa umma kuhusu mfumo huu wa 2-6-6-3.Serikali, vilevile, ihakikishe kuwa wanafunzi kutoka maeneo au familia maskini hawaachwi nyuma. Kulingana na mfumo wa sasa wa 8-4-4, wazazi wanalipa karo kwa miaka minne katika shule ya sekondari.

Lakini mtaala mpya wa 2-6-6-3, sekondari itakuwa na miaka sita – wanafunzi watasoma Sekondari ya Chini (JSS) kwa miaka mitatu na Sekondari ya Juu (SSS) miaka mitatu.

Serikali iondoe karo katika shule ya msingi (kuanzia Gredi 1 hadi Gredi 6) na masomo ya JSS ili kuwapunguzia wazazi mzigo wa kulipa karo kwa miaka sita.

You can share this post!

Bei ya mafuta kupandisha gharama ya maisha

TAHARIRI: Tumbo lisiongoze maamuzi ya BBI