LEONARD ONYANGO: Hakuna mwananchi mdogo wala mkubwa

LEONARD ONYANGO: Hakuna mwananchi mdogo wala mkubwa

Na LEONARD ONYANGO

KATIKA ulingo wa siasa, hivi karibuni kumekuwa na mjadala mkali kuhusu ‘Wakubwa’ na ‘wananchi wadogo’. Kwa mujibu wa wanasiasa wanaoendeleza mjadala huu, Wakenya wa tabaka la chini au walalahoi ndio ‘wananchi wadogo’ na mabwanyenye walio na ushaiwishi serikalini ndio ‘wakubwa’.

Naibu wa Rais William Ruto katika kampeni zake anapojinadi kwa ajili ya kinyang’anyiro cha urais 2022, amekuwa akisema kuwa analenga kusaidia ‘wananchi wadogo’ kujiinua kiuchumi endapo atachaguliwa kuwa rais wa tano wa Kenya.

Kwa mujibu wa Naibu wa Rais, wahudumu wa bodaboda, mama mboga, watu wa mkokoteni, juakali pamoja na Wakenya wengineo wanaotokwa na jasho katika harakati za kusaka tonge, ndio ‘wananchi wadogo’.

Dkt Ruto ambaye amejigeuza mtetezi wa ‘mahasla’ yaani walalahoi, anasema kuwa anaandaa mfumo wa uchumi utakao anzia chini mwa ‘wananchi wadogo’ kabla ya kuelekea juu kwa wakubwa.

Msemo wa ‘wananchi wadogo’ hautumiwi na Dkt Ruto pekee bali umezoeleka katika midomo ya wanasiasa wengi. Kwenye ulingo wa siasa pia kumekuwa na msemo mwingine: ‘wananchi wa kawaida’ – kurejelea Wakenya maskini hohehahe wanaoishi kwa kudra ya Mungu.

Mabwanyenye pamoja na wanasiasa ni Wakenya wasio wa kawaida labda kwa sababu wanaishi kwenye majumba ya kifahari, wanaenda katika hospitali za viwango vya juu, watoto wao wanasomea katika shule za kimataifa na akaunti zao za benki zimesheheni mamilioni ya fedha.

Udunishaji

Maneno ‘wananchi wadogo’ au ‘Wakenya wa kawaida’ yanadunisha Wakenya ambao wanajitahidi kila asubuhi kujitafutia riziki halali kwa jasho lao.Inawezekana kwamba huenda baadhi ya wanasiasa wanatumia maneno hayo kurejelea Wakenya wa mapato ya chini.

Hata hivyo, matendo ya wanasiasa wengi yanaashiria kuwa hawajali Mkenya wa tabaka la chini.Inaonekana dhana hii potovu ndiyo inasababisha mabwanyenye – ambao wengi wao wanashikilia nyadhifa kuu katika serikali ya kitaifa na kaunti – kupora fedha za kujengea hospitali au kununulia dawa za kutibu wananchi wadogo.

Dhana hii potovu ndiyo huchangia mabwanyenye kuacha watoto wa maskini kusomea chini ya miti huku wana wao wakisomea kwenye shule za kifahari.

Kasumba hiyo ya kudunisha wananchi wa mapato ya chini ndiyo inafanya mabwanyenye kutoa ahadi hewa wakati wa kampeni za uchaguzi kisha wanapochaguliwa hushughulikia maslahi yao ya kibinafsi bila kujali wapigakura.

Kwa mujibu wa Katiba, Wakenya wote ni sawa – hakuna Mkenya mdogo wala mkubwa. Mtoto wa maskini anahitaji elimu bora sawa na mtoto wa tajiri au wakuu serikalini.

Mtoto wa maskini anahitaji maji safi na salama sawa na mtoto wa bwanyenye na wanasiasa. Mtoto wa maskini anahitaji makazi bora sawa na mtoto wa wanasiasa. Kuna haja kwa wanasiasa kuepuka maneno haya yanayodunisha maskini. Sisi sote machoni pa Mungu na katiba tu sawa.

  • Tags

You can share this post!

China yahimiza huduma bora za kulinda watoto wakitoka...

WANTO WARUI: Serikali iokoe wanafunzi wanaotaabika Mbeere...