LEONARD ONYANGO: Rais aingilie kati, azime joto kali la kisiasa nchini

LEONARD ONYANGO: Rais aingilie kati, azime joto kali la kisiasa nchini

Na LEONARD ONYANGO

MATUKIO ya hivi karibuni ambapo makundi ya vijana yamekuwa yakivuruga mikutano ya wanasiasa wakuu kwa kurusha mawe, yanafaa kushtua Wakenya.

Wiki iliyopita kundi la vijana lilivuruga msafara wa kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga aliyekuwa akipigia debe mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) katika eneo la Githurai, Nairobi.

Vijana waliokuwa wakiimba, “Tunataka Ruto. Tunataka Ruto,” walishambulia kwa mawe msafara wa Bw Odinga huku watu kadhaa wakijeruhiwa katika ghasia hizo.

Siku moja baadaye, msafara wa Naibu Rais, Dkt William Ruto ulishambuliwa katika soko la Burma, Nairobi, na vijana waliokuwa wakiimba, “Tunataka BBI”.

Matukio hayo yamepandisha joto la kisiasa nchini na sasa Wakenya wameanza kuishi kwa hofu. Joto hilo la kisiasa ni hatari kwa amani na biashara nchini.

Iwapo serikali haitachukua hatua za haraka kuzima joto hilo, huenda tukaanza kushuhudia watu wakihama kutoka baadhi ya maeneo kwa kuhofia kushambuliwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2022 kama ilivyokuwa baada ya uchaguzi wa 2007.

Mara baada ya kisa cha kwanza cha virusi vya corona kuthibitishwa humu nchini, kaunti mbalimbali zilifunga masoko na mamilioni ya Wakenya wakapoteza biashara zao.

Ripoti ya Shirika la Takwimu nchini (KNBS) zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya wafanyabiashara wa kiwango kidogo kama vile mamamboga na juakali ndio wameathiriwa zaidi na janga la corona.

Mamilioni wamepoteza biashara zao na sasa wanahangaika.Baada ya hali kuonekana kutulia, baadhi ya wafanyabiashara sasa wameanza kujiinua ili kurejelea hali yao ya awali.

Lakini joto jingi la kisiasa linalozidi kupanda nchini huenda likawa pigo kwao.Idadi kubwa ya wazazi wanaohamisha watoto wao kutoka katika shule za kibinafsi hadi shule za umma kutokana na ukosefu wa karo ni ishara ya kuonyesha jinsi Wakenya walivyoathiriwa na janga la corona.

Kinaya ni kwamba Dkt Ruto na Bw Odinga wote wamekuwa wakidai kuwa wanapigania maslahi ya Wakenya maskini. Ikiwa kweli wanajali maskini, wasitishe kampeni zao za mapema ili kuwapa Wakenya wa mapato ya chini fursa ya kujiinua kibiashara.

Inasikitisha kuwa wanasiasa hao wameanza kampeni za 2022 ilhali imesalia takriban miezi 18 kabla ya Uchaguzi Mkuu. Wakenya hawali siasa!Wanasiasa wanaomezea mate viti vya ugavana, udiwani, ubunge, useneta na uwakilishi wa wanawake katika kaunti mbalimbali nchini huenda pia wakaanza kutumia ghasia ili kutishia wapinzani wao.

Hii ni kwa sababu serikali imefumbia macho vurugu ambazo zimeshuhudiwa katika mikutano ya Dkt Ruto na Bw Odinga. Mbona vigogo wanaofadhili vurugu hizo hawajakamatwa?

Rais Uhuru Kenyatta amenukuliwa mara kadhaa akisema kuwa anataka kukumbukwa kama rais aliyeacha Wakenya wakiwa wameungana atakapostaafu 2022.

Lakini kwa kushindwa kuzima joto la kisiasa ambalo limeanza kutishia amani, Rais Kenyatta huenda akaingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kama kiongozi wa nchi atakayeacha taifa likiwa limegawanyika kwa kiwango cha juu.

You can share this post!

Bodaboda wapiga teke punda Lamu

WANTO WARUI: TSC imejifunga kibwebwe kuporomosha KNUT...