LEONARD ONYANGO: Serikali ina mengi ya kujifunza kuhusu elimu

LEONARD ONYANGO: Serikali ina mengi ya kujifunza kuhusu elimu

Na LEONARD ONYANGO

TANGU kufunguliwa kwa shule Januari 4, mwaka huu, baada ya watoto kukaa nyumbani kwa karibu miezi kumi kufuatia janga la virusi vya corona, kuna mambo mengi ambayo serikali inafaa kujifunza.

Funzo la kwanza ni kuwa kuna haja kwa serikali kuongeza idadi ya shule za umma.Waziri wa Elimu Profesa George Magoha hivi majuzi alikiri kuwa baadhi ya shule za umma zimelemewa na idadi kubwa ya wanafunzi.

Waziri aliwataka wazazi wanaotaka kuhamishia watoto wao katika shule za umma kuwasilisha maombi yao kwa maafisa wa elimu wa kaunti ndogo.

Prof Magoha alisema kuwa msongamano huo katika shule za umma umesababishwa na wanafunzi ambao wamekuwa wakihama kutoka shule za kibinafsi ambazo zilikosa kufunguliwa kutokana na makali ya janga la virusi vya corona. Msongamano huo ni ithibati kuwa serikali inafaa kujenga shule za umma za kutosha kwa dharura.

Kwa miaka mingi serikali imelaza damu na imeachia shule za kibinafsi jukumu la kuelimisha watoto.Kwa mfano, katika eneobunge la Roysambu, Kaunti ya Nairobi, kuna shule moja pekee ya msingi ya umma licha ya kuwa na wakazi 200,000.

Mafuriko ambayo yamesababisha uharibifu wa majengo ya shule katika maeneo mbalimbali ya nchi yametia msumari moto kwenye kidonda.

Hali imekuwa mbaya zaidi kwa sababu ripoti kuhusu Hali ya Uchumi ya 2020 iliyoandaliwa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS) inaonyesha kuwa idadi ya shule humu nchini inazidi kupungua badala ya kuongezeka.

Ripoti ya KNBS inaonyesha kuwa shule za umma za msingi zilipungua kutoka 24,241 mnamo 2018 hadi 23,286 mwaka wa 2019.Katika kipindi sawa, ripoti hiyo inaonyesha kuwa shule za msingi za kibinafsi zilipungua kutoka 13,669 hadi 9,058.Shule za sekondari za umma zilipungua kutoka 9,643 hadi 8,933.

Huku za kibinafsi zikipungua kutoka 1,756 hadi 1,530.Kulingana na ripoti ya KNBS, shule za chekechea ndizo zinaongezeka. Kati ya 2018 na 2019, shule za chekechea ziliongezeka kutoka 25,589 hadi 28,383.Jambo la pili ambalo serikali inafaa kujifunza ni kuhusu athari za janga la virusi vya corona nchini.

Kulingana na wizara ya Elimu, kati ya Januari 4 na Januari 7, wanafunzi 10,000 waliokuwa wakisomea katika shule za kibinafsi walikuwa tayari wamesajiliwa katika shule za umma.

Wengi wa wazazi wamehamishia watoto wao katika shule za umma baada ya kushindwa kulipa karo katika shule za kibinafsi.Idadi hiyo kubwa ya wanafunzi wanaohamia katika shule za umma kutoka shule za kibinafsi inadokeza jinsi janga la corona limesababisha mamilioni ya Wakenya kuishi maisha ya uchochole.

Serikali inafaa kuelekeza nguvu zake katika kuweka mazingira murua kuwawezesha Wakenya waliopoteza ajira au biashara zao kujiinua tena.Aidha, serikali inafaa kuweka mikakati mwafaka kuhakikisha kuwa zaidi ya watoto 500,000 ambao hawajarejea shuleni tangu shule zilipofunguliwa wiki iliyopita, wanatafutwa na kurudishwa shuleni.

You can share this post!

Njama ya Joho, Kingi ‘kupiga chobo’ vinara wa Tangatanga

WANTO WARUI: Kuzuia wanahabari shuleni kunaficha maovu