LEONARD ONYANGO: Ukweli ni kuwa Kenya yahitaji suluhu ya madeni

LEONARD ONYANGO: Ukweli ni kuwa Kenya yahitaji suluhu ya madeni

Na Leonard Onyango

WAKENYA, wiki iliyopita, walitumia mitandao ya kijamii kushinikiza Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kufutilia mbali mkopo wa Sh255.1 bilioni uliotolewa siku 10 zilizopita kupambana na madhara ya janga la virusi vya corona.

Kenya italipia mkopo huo ndani ya miezi 38 ijayo. Mkopo huo ulifanya deni ambalo Kenya inadaiwa kufikia Sh7.25 trilioni. Hiyo inamaanisha kuwa kila Mkenya anadaiwa takribani Sh150,000.

IMF pia, wiki iliyopita, ilifichua kwamba Kenya inalenga kukopa Sh1.3 trilioni zaidi ndani ya miezi 18 ijayo; na kufanya deni kufikia takribani Sh8.5 trilioni. Hiyo inamaanisha kuwa walipa ushuru watalazimika kujifunga kibwebwe kulipa mikopo hiyo.

Rais Uhuru Kenyatta atakapostaafu Agosti mwaka ujao, atasalia kwenye daftari la kumbukumbu kwa kuwa kiongozi wa nchi aliyeacha wananchi wakichechemea kwa mzigo mkubwa wa madeni ambayo yatachukua miaka mingi kabla ya Wakenya kupata afueni.Wakenya, wiki iliyopita, walitumia mitandao ya kijamii wakiwa na imani kwamba malalamishi yao yangesikilizwa na IMF.

Lakini baadaye, IMF ilisema kwamba Kenya iko pabaya na haiwezi kustawi bila kuchukua mikopo ya shirika hilo. Japo sehemu ya fedha zinazokopwa zinatumiwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kiasi kikubwa kinaishia katika mifuko ya wachache.

Majuzi, Rais Kenyatta alikiri kuwa Sh2 bilioni fedha za umma huibwa kila siku na watu ambao hakuwataja.Serikali ilionekana kukerwa na kampeni ya kuitaka IMF kusitisha mikopo – hatua iliyosababisha wanaharakati wakiongozwa na Edwin Kiama kukamatwa.

Bw Kiama alifikishwa mahakamani Alhamisi lakini akaachiliwa Ijumaa kwa dhamana ya Sh500,000.Wanasiasa na wataalamu wanaoegemea upande wa serikali, walipuuzilia mbali kampeni ya kuitaka IMF kusitisha mikopo kwa Kenya huku wakisema kuwa wanaopinga wanapoteza wakati.

Walidai kuwa IMF haikubali malalamishi kupitia mitandao ya kijamii.Baadhi yao, pia walishutumu Wakenya kwa kupinga mikopo ilhali wao wamezongwa na mikopo ambayo huwa wanachukua kwa njia ya simu.Ni kweli kwamba IMF haiwezi kutumia mitandao ya kijamii kufanya maamuzi yake.

Lakini malalamishi hayo ya Wakenya yalisheheni ujumbe mzito ambao haufai kupuuzwa na Rais Uhuru Kenyatta.Malalamishi hayo yalionyesha kuwa Wakenya wamechoka kutwikwa mzigo mzito wa madeni.

Malalamishi hayo yaliashiria kuwa walipa ushuru wanaumia na wanahitaji kupumzika.Wananchi wanahangaika kwa kutozwa ushuru wa juu kupindukia.

Mikopo ya simu ambayo Wakenya wamesakamwa nayo inatokana na hali ngumu ya uchumi.Malalamishi hayo pia ni ishara kwamba Wakenya wako tayari kuchagua kiongozi atakayetoa suluhu kwa suala la mzigo mzito wa madeni.Wanasiasa wanaomezea kiti cha urais 2022 wawaeleze wapigakura namna watakavyoshughulikia madeni yaliyoizonga Kenya.

You can share this post!

Wakenya waendelea kuishinikiza IMF kukoma kuikopesha Kenya

Waziri Mkuu asema hatahudhuria mazishi ya mume wa Malkia...