LEONARD ONYANGO: Wapigakura wajifunze kutoka ahadi feki 2017

LEONARD ONYANGO: Wapigakura wajifunze kutoka ahadi feki 2017

Na LEONARD ONYANGO

MSIMU wa wanasiasa kumwaga ahadi hewa umeanza. Kila mwanasiasa anajifanya kuwa ‘mwokozi’ wa Wakenya maskini.

Huku kinara wa ODM Raila Odinga akidai kuwa atafanya Kenya kufurika kwa viwanda na kila Mkenya atapata ajira ikiwa atachaguliwa kuwa rais 2022, Naibu wa Rais William Ruto, kwa upande mwingine, ameshikilia kuwa umaskini utaisha Kenya kwani walala hoi (mahasla) wote watapata usaidizi kutoka kwa serikali.

Kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi anasema wafanyabiashara wadogo wataondolewa ushuru na Kenya haitadaiwa na mataifa ya kigeni iwapo atachaguliwa kuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta mwaka ujao.

Ahadi sawa na hizo pia zimekuwa zikitolewa na wanasiasa wanaomezea viti mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Wakenya milioni 23.4 ni maskini wa kutupwa na asilimia kubwa ya waliosalia wanaishi kwa kubangaiza, kwa mujibu wa ripoti kuhusu hali ya umaskini nchini iliyotolewa mwaka jana na Shirika la Takwimu nchini (KNBS).

Wanasiasa wanamezea mate kura za maskini hao ambao wamekuwa wakirauka alfajiri kupanga foleni kupiga kura kila baada ya miaka mitano kutokana na matumaini kwamba huenda masaibu yao yakaisha.

Lakini wanaendelea kuzama kwenye umaskini na maisha yanazidi kuwa magumu.Mnamo Juni 2017, mwaniaji wa ugavana wa Kaunti ya Nairobi Mike Mbuvi Sonko pamoja na mwaniaji mwenza Polycarp Igathe, waligeuka vipenzi vya wapigakura baada ya kutangaza ahadi tele zilizolenga kumaliza umaskini jijini.

Wakati wa uzinduzi wa manifesto yake, Bw Sonko alitangaza kuwa angepunguza kwa asilimia 50 ada ya kuegesha magari jijini Nairobi iwapo angechaguliwa kuwa gavana.Wakati huo, ada ya kuegesha gari kwa siku ilikuwa Sh200.

Ahadi hiyo ya Bw Sonko inamaanisha kuwa wenye magari wangelipa ada ya Sh100.Sonko pia alisema kuwa angefutilia takwa la wafanyabiashara wadogo jijini Nairobi kuwa na leseni ya biashara zao.

Seneta huyo wa zamani wa Nairobi pia alisema kuwa endapo angechaguliwa angefutilia mbali ushuru unaotozwa wafanyabiashara katika mitaa ya mabanda.

Wafanyabiashara wadogowadogo jijini Nairobi pia hawakufaa kulipa ushuru chini ya uongozi wa Sonko.Ahadi hizo zote zilifaa kutekelezwa ndani ya siku 100 za uongozi wa wawili hao.

Idadi kubwa ya wakazi wa Nairobi ni maskini na wanahangaika kupata mahitaji muhimu, ikiwemo chakula.

Asilimia kubwa ya wanaomiliki magari jijini Nairobi wanalazimika kuyaacha majumbani kutokana ada ya juu ya kuegesha magari katikati mwa jiji.

Hawa ndio Bw Sonko alilenga na walimpigia kura kwa wingi na akaibuka mshindi baada ya kumbwaga aliyekuwa Gavana Evans Kidero.

Lakini baada ya kuchaguliwa, mambo yalibadilika. Ada ya kuegesha magari katikati mwa jiji ilipandishwa kutoka Sh200 hadi Sh300.

Vibanda vya wafanyabiashara wadogowadogo vilibomolewa. Takataka ilitapakaa kila kona na wafanyabiashara katika mitaa ya mabanda waliendelea kulipa ushuru.

Maisha ya wakazi wa Nairobi yalizidi kuwa magumu badala ya kupata afueni.Hiyo ndiyo maana Sonko alipotimuliwa na madiwani mwaka jana, hakuna mtu alijitokeza kuandamana.

Wakazi wa Nairobi walikuwa wamechoshwa na uongozi wake.Wanasiasa wanaotoa ahadi kubwa kubwa sasa hawana tofauti na Bw Sonko.

You can share this post!

Wakazi wavamia kasisi anayedaiwa kulawiti wavulana

WANTO WARUI: Tutahadhari kuhusu corona Kidato cha Kwanza...