LEONARD ONYANGO: Wawaniaji urais walipe uzito suala la mabadiliko ya tabianchi

LEONARD ONYANGO: Wawaniaji urais walipe uzito suala la mabadiliko ya tabianchi

Na LEONARD ONYANGO

HUKU Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022 ukinukia, wanasiasa wanaomezea mate urais wamekuwa wakizunguka kila pembe ya nchi wakihubiri miujiza kuhusu namna watakavyomaliza umaskini nchini Kenya iwapo watachaguliwa.

Baadhi yao wameahidi namna watakavyopeleka mamilioni ya fedha kwa kila eneobunge ili kusaidia kuinua biashara za Wakenya wa tabaka la chini, wakiwemo ‘mama mboga’, wahudumu wa bodaboda.

Wengine wameahidi kuhakikisha kuwa kila Mkenya anashiba na njaa itasalia katika vitabu vya historia iwapo watachaguliwa.

Naibu wa Rais William Ruto, kwa mfano, Wakenya maskini wanaostahili usaidizi wa dharura ni ‘mama mboga’, wahudumu wa bodaboda na wasukuma mikokoteni.

Lakini ukweli ni kwamba maskini wanaohitaji msaada zaidi kutoka kwa serikali ni wakulima wanaozalisha mboga au nyanya zinazouzwa na hao mama mboga.

Ikiwa mama mboga jijini Nairobi anauza nyanya moja kwa Sh10, hiyo ina maana kwamba mkulima aliiuza kwa chini ya Sh4.

Je, kati ya wawili hao nani anaumia zaidi?Nyingi ya nyanya au mboga zinazotumiwa nchini, zinazalishwa na wakulima wadogo wanaohangaishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile ukame, mafuriko, wadudu na magugu.

Sekta ya kilimo imesaidia asilimia 75 ya Wakenya kupata ajira, kulingana na takwimu za wizara ya Kilimo. Sekta hiyo inachangia asilimia 25 ya mapato ya nchi (GDP).

Kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi alipozindua mikakati yake Ijumaa iliyopita kuhusu anavyopanga kuinua uchumi nchini iwapo atachaguliwa kuwa rais, alisema kuwa ataboresha hali ya uchumi wa wafugaji haswa katika maeneo kame – ambayo ni sawa na asilimia 80 ya Kenya.

Lakini Bw Mudavadi hakuelezea jinsi atawasaidia wafugaji hao kukabiliana na makali ya tabianchi. Wafugaji wanahitaji kusaidiwa na serikali kupata bima ya mifugo yao ili wakifa wakati wa ukame walipwe fidia.

Vilevile, wanahitaji maji ambayo yatafaa mifugo wao wakati wote.Sekta ya kilimo inakabiliwa na changamoto tele zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kama vile ukame na mafuriko ya mara kwa mara.

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Chakula (FAO) iliyotolewa miezi miwili iliyopita inaonyesha kuwa magugu na wadudu wanaoharibu mazao wataongezeka nchini katika miaka ijayo kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Benki ya Dunia inakadiria kuwa idadi ya watu watakaoathiriwa na ukame nchini Kenya itaongezeka kwa kati ya asilimia 10 na 17 kufikia 2030.

Idadi ya watu watakaoathiriwa na mafuriko itaongezeka kwa asilimia 10-15 ndani ya miaka minane ijayo.

Asilimia 98 ya kilimo nchini Kenya inategemea mvua na hiyo inamaanisha kuwa kiwango cha umaskini kitaongezeka nchini.

Kusaidia mama mboga na bodaboda si suluhisho la umaskini nchini.Wanasiasa wanaoahidi kumaliza umaskini nchini bila mipango kabambe ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi wapuuzwe.

You can share this post!

CECIL ODONGO: Kuna dalili uchaguzi wa 2022 huenda urudiwe

Itikadi na miko ya Uswahilini ambayo haihusiani na dini