Michezo

Leopards, Bandari na Kakamega Homeboyz waanza vyema kampeni za FKFPL

November 28th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA mara 13 wa Ligi Kuu ya Kenya, AFC Leopards, walianza vyema kampeni za kuwania taji la msimu huu wa 2020-21 kwa kuwapokeza Tusker FC kichapo cha 2-1 uwanjani Nyayo, Nairobi mnamo Novemba 28, 2020.

Kikosi hicho cha kocha Tomas Trucha kilitoka nyuma na kufungiwa na Robinson Kamura na Elvis Rupia katika dakika za 26 na 34 mtawalia.

Tusker ya kocha Robert Matano ndio waliotangulia kuona lango la Ingwe kupitia David Majak aliyefungia mabingwa hao mara 11 katika dakika ya 22.

Kwingineko, Kakamega Homeboyz wanaonolewa na mkufunzi Nicholas Muyoti waliwapepeta limbukeni Vihiga United 1-0 uwanjani Mumias Sports Complex.

Matokeo sawa na hayo yalivunwa na Bandari FC dhidi ya Sofapaka uwanjani Mbaraki, Mombasa.

David Odhiambo aliwafungia Homeboyz bao la pekee na la ushindi katika dakika ya 47 kabla ya Henry Juma wa Vihiga kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 68. Goli lililowapa Bandari alama tatu muhimu lilifumwa wavuni na Abdallah Hassan katika dakika ya 20 baada ya kushirikiana vilivyo na Yema Mwana na David King’atua.