Michezo

Leopards na Nzoia zatamba, Rangers ikishuka zaidi KPL

April 9th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

AFC Leopards na Nzoia Sugar ndizo klabu zilizoimarika zaidi kwenye jedwali la Ligi Kuu baada ya mechi za raundi ya 21 kusakatwa wikendi.

Mabingwa mara 13 Leopards, ambao mwezi mmoja uliopita walikuwa ndani ya mduara hatari wa kutemwa, wameendelea kujiondoa karibu na maeneo hayo kabisa baada ya kuchapa Ulinzi Stars 1-0 Jumapili na kuruka juu nafasi mbili hadi nambari 10.

Vijana wa Casa Mbungo wana alama 26. Wako alama moja mbele ya Nzoia ambao pia wamepia hatua mbili mbele kufuatia ushindi wao wa mabao 6-1 dhidi ya Mount Kenya United.

Kocha Casa Mbungo wa klabu ya AFC Leopards. Picha/ Maktaba


Mabingwa wa mwaka 2006 SoNy Sugar pia wako katika orodha ya timu tatu zilizotia fora baada ya kupata ushindi wao wa tatu mfululizo dhidi ya Posta Rangers kwa kuwalemea 2-1.

SoNy wameruka juu nafasi moja hadi nambari saba.

Wamezoa alama 31. Hakuna mabadiliko katika nafasi tatu za kwanza ambapo Gor Mahia inaongoza kwa alama 44. Uongozi wa Gor wa alama saba, hata hivyo, ulikatwa hadi nne baada ya washindi wa mwaka 2009 Sofapaka kuzaba Zoo 2-0.

Gor bado ina mechi mbili mkononi. Imezoa alama 44. Huenda ikacheza mechi moja ligini kabla ya kuelekea nchini Morocco kwa mechi ya marudiano ya Kombe la Mashirikisho la Bara Afrika dhidi ya Berkane. Ilichapwa 2-0 uwanjanio Kasarani Jumapili.

Bandari inasalia katika nafasi ya tatu kwa alama 39, moja nyuma ya Sofapaka iliozamisha Kariobangi Sharks 1-0. Wafalme wa mwaka 2008 Mathare United wamekwamilia nafasi ya nne kwa alama 35 baada ya kukubali sare ya 1-1 dhidi ya washindi mara 11 Tusker.

Kakamega Homeboyz ni ya tano kwa alama 33 baada ya kuandikisha ushindi wao wa nne mfululizo wakichabanga Chemelil Sugar 2-0. Nambari sita ni Tusker, ambao wamezoa alama 31 sawa na SoNy nayo Sharks iko alama moja nyuma katika nafasi ya nane.

KCB, ambayo imerejea Ligi Kuu baada ya kuwa ligi ya daraja ya pili misimu mitatu, wanashikilia nafasi ya tisa kwa alama 29. Walipata alama tatu katika raundi ya 21 kwa kuliza Vihiga United 3-0. Leopards wanafunga mduara wa 10-bora.

Ulinzi iko chini nafasi mbili hadi nambari 12 kwa alama 25. Western Stima, ambao walianza msimu vyema na hata kuonekana wagombeaji halisi wa taji baada ya kurejea kutoka ligi ya daraja ya pili, wanaendelea kuteremka chini ya jedwali. Wanaumeme hawa wanashikilia nafasi ya baada ya kushuka nafasi mbili.

Wanashikilia nafasi ya 13 kwa alama 25. Ulinzi na Stima wamecheza mechi 20 kila mmoja.
Chemelil, Vihiga na Rangers wamesalia katika nafasi za 14, 15 na 16 wakiwa na alama 21, 20 na 17, mtawalia.

Zoo, ambayo haina ushindi katika mechi tano, imesalia katika nafasi ya 17 kwa alama 17. Imefungwa mabao mengi kuliko Rangers. Baada ya kupoteza mechi sita mfululizo, Mount Kenya iliyoponea chupuchupu kutupwa katika Ligi ya Supa msimu uliopita, inasalia mkiani kwa alama 12 kutokana na mechi 21.