Michezo

Leopards yazindua app ya mashabiki kuchangia timu

August 30th, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

AFC Leopards imeanzisha programu ya simu ya mkononi ambapo mashabiki watumia kujiandikisha kama wanachama.

Akitangaza habari hizo jana katika hafla ya kuuzindua rasmi mpango huo, Dan Shikanda ambaye kuchaguliwa kwake kama mwenyekiti wa klabu hiyo kunachunguzwa, alisema programu hiyo itaiwezesha Ingwe kujipatia pesa baada ya SportPesa kujiondoa ghafla kama wadhamini.

Shikanda ambaye aliwahi kuchezea klabu hiyo pamoja na timu ya taifa ya Harambee Stars, alikuwa akiwahutubia mashabiki akiwemo Mbunge wa Makadara George Aladwa na aliyekuwa kocha wa Harambee Stars, Jacob ‘Ghost’ Mulee, Jumatano usiku katika uzinduzi rasmi wa mpango huo uliofanyika ukumbini Charter Hall, Nairobi.

Alieleza kuwa kamati yake inanuia kuandikisha wanachama 100,000 kutoka pembe zote duniani ambao kwa jumla inalenga kupata Sh100 milioni kila mwaka.

“Wadhamini wetu wamekuwa wakitupatia Sh52 milioni kwa mwaka, kikiwa kiwango kidogo zaidi kugharimia matumizi yetu, ikizingatiwa kwamba bajeti yetu ni Sh100 milioni kwa mwaka,” alieleza.

“Sasa tumeamua kujitegemea, na sasa mpango huu unatupa fursa ya kujifanyia mambo na kujitegemea milele.”

Aladwa ambaye aliwahi kuhudumu kama katibu mkuu wa klabu hiyo na baadaye kama naibu mwenyekiti, aliupongeza mpango huo aliosema unapaswa kuungwa mkono na mashabiki wote wa Ingwe.

“Wakati wetu, kiasi kikubwa cha pesa kilipatikana kutokana na malipo ya langoni, lakini baadhi yetu walikuwa na tamaa ya kuzitumia pesa hizo vibaya bila kujali maslahi ya wachezaji, lakini sasa hakuna atakayenyanyasa wachezaji tena.”

Kutuma pesa

Wakati wa hafla, kocha Casa Mbungo aliwaomba mashabiki wa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kujitolea kutuma chochote walicho nacho ili wasaidie wachezaji ambao wanalenga kumaliza katika nafasi nzuri kuliko ilivyokuwa msimu uliopita. Leopards ilimaliza katika nafasi ya 11 katika ligi hiyo inayojumuisha timu 18.

Kulingana na mpango huo wa wanachama watapenyeza nambari *417# kwenye simu zao na na kufuata utaratibu.

“Jameni wacheni kuendelea kuunga mkono timu za ng’ambo. Jitokezeni viwanjani tushangilie timu zetu kwa lengo la kuimarisha mchezo huu nchini,” aliuongeza Mulee.

Katika mpango huo, wanachama watapata fursa ya kujiandikisha kwa siku na pia kwa mwezi mzima kuanzia kiasi cha Sh10, kadhalika watautumia mpango huo kujiandikisha kama wanachama wa mwaka, kujinunulia mavazi ya timu na tiketi za kwenda uwanjani kushuhudia mechi za timu yao.

Leopards imepangiwa kuanza na Kakamega Homeboyz Jumapili ugenini Bukhungu Stadium katika mechi yao ya kwanza ya msimu huu wa 2019/2020.