Leteni hoja hiyo tupambane nayo, Tangatanga waambia Savula na wenzake

Leteni hoja hiyo tupambane nayo, Tangatanga waambia Savula na wenzake

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wandani wa Naibu Rais William Ruto wameapa kuzima hoja ya kumwondoa mamlakani endapo itawasilishwa bungeni mara bunge litakaporejelea vikao vyake kuanzia Jumanne, Februari 9, 2021.

Wakiongea na wanahabari Jumatano katika makao ya Dkt Ruto katika mtaa wa Karen, wabunge hao 139 wamemtaka Mbunge wa Lugari Ayub Savula anayepanga kuwasilisha hoja hiyo kukoma kujadili suala hilo katika maeneo mengine kando na bunge.

“Wakome kujadili suala la kutimuliwa kwa Naibu Rais katika hafla za mazishi, baa na katika nyumba za wapenzi wao. Walete mswada huo bungeni kesho (Jumanne) bunge litakaporejelea vikao vyake baada ya likizo ndefu,” akasema Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale.

Bw Duale ambaye amehudumu kama kiongozi wa wengi bungeni kuanzia 2013 hadi Juni 2021 amesema kuwa mchakato wa kumwondoa mamlakani Naibu Rais sio suala jepesi anavyodhani Bw Savula na “wadhamini wake”.

Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale. Picha/ Charles Wasonga

“Tunawaambia waulete tuko tayari kukabiliana na wao. ANC, ODM, Wiper na Kieleweke; tafadhali nendeni mketi pahala fulani na muandae hoja hiyo vilivyo kisha muilete bungeni. Tuko tayari kupambana na ninyi,” akasema Bw Duale huku akionekana amekunja uso.

Naye Seneta wa Meru Mithika Linturi amesema wakati huu hawawezi kusema lolote kuhusu mswada huo kwani hoja hiyo haijawasilishwa rasmi katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

“Waiandae na wailete bungeni. Wakati huu sisi kama muungano wa wabunge wandani wa Naibu Rais hatuwezi kusema lolote kuhusu suala hilo,” akasema.

Waliongea baada ya mkutano wa mashauriano wa wabunge wa mrengo wa ‘Tangatanga’ uliofanyika katika makazi ya Dkt Ruto mtaani Karen, Nairobi. Dkt Ruto mwenyewe ndiye ameongoza mkutano huo ambao umehudhuriwa na wabunge na maseneta 139.

Mnamo Jumapili Bw Savula alisema kuanzia Jumanne atakusanya sahihi za wabunge wanaounga mkono hoja hiyo huku akisema kuwa suala hilo linaungwa mkono na vigogo wakuu wa vyama vya Jubilee na ODM.

Hata hivyo, mnamo Jumatatu, Februari 8, 2021, Katibu Mkuu wa Jubilee amesema chama hicho hakina mpango wowote wa kudhamini hoja ya kumng’oa mamlakani Dkt Ruto.

You can share this post!

Maseneta sita wa Jubilee watimuliwa kwa ukaidi

Sonko adai kuna mtu alitaka kumdunga sindano ya sumu